Raia wa India aliyekuwa kiongozi wa hotel ya Ramada iliyoko eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam ametumbuliwa jipu baada ya kuwaita wafanyakazi wa ngazi ya chini ‘nyani’.

Mhindi huyo aliyetajwa kwa jina la Dennis Smith anadaiwa kuwashambulia wafanyakazi hao kwa lugha chafu na maneno ya kibaguzi siku ya Valentine (Februari 14), baada ya kuwashutumu kwa kushindwa kuandaa vizuri meza kwa ajili ya wateja.

Wakiongea na waandishi wa habari jana, wafanyakazi wa hoteli hiyo kubwa walieleza kuwa kufutia kauli mbaya na unyanyasaji wanaofanyiwa na Smith ambaye ni Meneja wa vyakula na vijwaji, waliamua kugoma kufanya kazi wakishinikiza aondolewe au wao waache kazi.

Naye Meneja Rasilimali watu wa hotel hiyo, Sebastian Nchimbi aliwaeleza waandishi wa habari kuwa tayari uongozi wa hotel umemuachisha kazi Meneja huyo ili kulinda wafanyakazi wake.

“Tulizungumza na wafanyakazi wakatuambia kuwa hawataki Smith awepo kazini na sisi tukafanya uamuzi ili kuwalinda wafanyakazi wetu,” alisema.

Nchimbi alikiri kupokea malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wafanyakazi kutokana na kauli mbaya za Smith na kwamba sasa wameamua kumuondoa rasmi.

Mwakilishi wa wafanyakazi wa hotel hiyo, Mathew Misalaba alieleza kuwa pamoja na hatua hiyo, wametoa taarifa kwa jeshi la polisi kumshtaki Smith kwa vitendo vyake vya kibaguzi ili achukuliwe hatua za kisheria.

 

Manispaa ya Kinondoni yabaini upotevu wa mabilioni, yawapa siku 7 wafanyabiashara
Tanzia: Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa afariki