Mpeperushaji bendera wa urais wa Muungano wa Azimio La Umoja One Kenya Raila Odinga amepata kura nyingi zaidi katika kituo cha kupigia kura cha Kigali, Rwanda.

Fomu ya 34A iliyochapishwa na vyombo vya Habari jijini Nairobi inaonyesha kuwa Odinga amepata kura 150, sawa na asilimia 62.7 ya kura zote zilizopigwa.

William Ruto wa UDA amekuwa wa pili kwa kupata kura 81, huku mgombeaji wa Roots Party, Profesa George Wajackoyah na wa chama cha Agano Waihiga David Mwaure wakipata kura 4 kila mmoja.

Wapiga kura 239 pekee walijitokeza kati watu 545 waliosajiliwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, ambapo Rwanda ni miongoni mwa nchi 12 ambazo tume hiyo ilifungua vituo vya kupigia kura ili kuwaruhusu Wakenya kushiriki katika kufanya uamuzi wao katika uchaguzi wa urais.

Zoezi la uhakiki wa wapigakura kwa njia ya kielektroniki pia linafanyika nchini Canada, UAE, Uingereza, Marekani, Qatar, Afrika Kusini, Ujerumani, Rwanda, Burundi, Uganda, Tanzania na Sudan Kusini.

Mgombea wa UDA, William Ruto akipiga kura Agosti 9, 2022.

Tume bado inapokea kura kutoka kwa vituo vingine vya Diaspora, huku wagombea wawili wa mbio za Urais William Ruto na Raila Odinga wakichuana vikali na tayari Wakenya wamefanya uamuzi wao Jumanne ya Agosti 9, 2022 na kinachosubiriwa sasa ni matokeo ya ujumla ambayo yanaendelea kuhesabiwa kote nchini humo.

Hata hivyo, Tume ya uchaguzi inatarajiwa kutangaza matokeo ya mwisho ya kura za urais ndani ya siku saba.

Young Africans yataja Kamati ya Mashindano
Bingwa wa CAF SUPER LEAGUE kulamba dola milioni 100