Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix-Antoine Tshisekedi Tshilombo amehutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani na kuzungumzia suala la amani na usalama mashariki mwa taifa lake, pamoja na harakati za kuinua uchumi wa nchi kupitia rasilimali zilizopo.

Tshisekedi, amehutubia mkutano huo Septemba 20, 2022 na kusema Umoja wa Mataifa unafahamu kuwa DRC ni muathirika wa janga kubwa la usalama, lililodumu Mashariki mwa nchi hiyo kwa zaidi ya miaka 20 akisema unatokana na rasilimali zilizopo ndani ya DRC ambazo ndiyo chanzo cha mzozo.

Amesema, “Mfuatiliaji yeyote wa dhati akizungumza kwa nia njema atakubaliana nami kuwa sababu sio nyingine ila ni ya mzozo unaoendelea Mashariki mwa DRC ukichochewa na rasilimali zilizomo ndani ya taifa letu na hata hivyo bado tunaweka jitihada za dhati ili kuweza kupata muafana na kuleta amani.”

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix-Antoine Tshisekedi Tshilombo. Picha na Digital Congo.

Aidha, amesema wananchi wa DRC wanatambua mchango wa Umoja wa Mataifa, Muungano wa Afrika, Jumuiya za kikanda za Afrika, Muungano wa Ulaya na wadau wengine katika kukabili janga hilo lilalojirudia mara kwa mara na kusema, “tunatambua kujitoa kwa walinda amani jasiri wa Umoja wa Mataifa, ambao wamepoteza maisha yao wakitetea maadili ya amani na haki.”

Hata hivyo amesema, licha ya juhudi za ndani, uwepo wa walinda amani wa UN wanaohudumu kwenye ujumbe wa Umoja huo, MONUSCO pamoja na msaada wa kidiplomasia kwa miaka 23, bado ukosefu wa usalama unazidi kutishia taifa lake.

Katika mkutano huo, Rais Tshisekedi ameuomba Umoja wa Mataifa, Muungano wa AFrika, Jumuiya za kikanda ya Afrika na wadau wa DRC kusaidia kujenga upya usalama, amani ya kudumu na kuweka mazingira bora ya ushirikiano wenye matunda kwa maslahi ya wakazi wote wa ukanda wa Maziwa Makuu.

Wizara ya Afya yatahadharisha ugonjwa wa Ebola
Viashiria uvunjifu wa amani vidhibitiwe: Majaliwa