Mgombea urais wa Chama cha Roots nchini Kenya Profesa George Wajackoyah ameahidi kutatua hali ya uchumi nchini humo kwa kutumia kifua iwapo atashinda kiti cha urais mnamo Agosti 9 na atakuwa dikteta.

Akizungumza siku ya Jumatatu, Julai 11, katika Jumba la Kitaifa la Mikutano KICC, katika Kongamano la Kitaifa la Uchaguzi la Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), amesema suala la uchumi wa Nchi linatakiwa kusimamiwa kwa umakini na kifua.

“Udikteta wa kiuchumi unasaidia na ninaweza kuwaambia Wakenya kuwa nitakuwa dikteta kuhusiana na uchumi wa nchi hii,” amesema.

Wajackoyah aliwalaumu wanasiasa kwa kushambuliana katika kampeni zao badala ya kupeleka ajenda yao kwa wapiga kura, akiwataka kuheshimiana, hasa wagombea urais na amewataka wakosoaji wake waache kudhani kuwa ni mwendawazimu na badala yake wamuombee abadilike na kuwa bora.

“Tuna amani, Hatutetei kuvuta sigara, Ninaweza kuonekana mwenda wazimu kwa sababu ya jinsi nilivyo, lakini nilizaliwa hivi. Tafadhali msinihukumu bali niombeeni nionekane bora kuliko vile mnavyotaka niwe, Mungu Aliniumba Hivi,” alisema.

Kama sehemu ya kampeni zake, Wajackoyah anatarajia kuhalalisha bangi kwa madhumuni ya kibiashara ili kulipa madeni pamoja na matumizi ya dawa pamoja na kuahidi kuwa serikali yake itaanzisha ufugaji wa nyoka na kusafirisha korodani na nyama ya mbwa nchini China ili kukuza uchumi.

Wajackoyah aliihakikishia jumuiya ya kimataifa kuhusu kujitolea kwake kufanya kazi pamoja ili kuendeleza ajenda ya maendeleo, akiwaondolea wasiwasi wawekezaji kwamba mipango yake itawaogopesha.

“Linapokuja suala la mahusiano ya kimataifa, hii sio sauti yangu, labda unaweza kufikiria kuwa nimevuta bangi. Sivuti kabisa. Sera yetu ya mambo ya nje itakuwa sera ya kutia moyo,” alisema.

Hata hivyo, alionyesha imani kuwa IEBC itafanya uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Zoran Maki: Nipo tayari kuikabili Young Africans
Mwingine kutambulishwa Simba SC