Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amekiri kuwa aliamuru Naibu Gavana wa Kilifi, Gideon Saburi akamatwe baada ya kuingia nchini humo akitokea Ujerumani na kukwepa karantini hali iliyoweka hatarini maisha ya Wakenya dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona (covid-19).

Akizungumza wakati wa mahojiano leo, Aprili 7, 2020, Rais Kenyatta amesema kuwa anamuombea kigogo huyo afungwe miaka 10 jela kwa uzembe wa makusudi wakati huu dunia ikipambana na covid-19.

“Mimi ndiye niliyesema Naibu Gavana wa Kilifi akamatwe, ninaomba apate kifungo cha miaka 10,” alisema Rais Kenyatta kwenye mahojiano hayo yaliyokaririwa na Daily Nation.

“Inawezekanaje kiongozi aruke kutoka Ujerumani na aanze kuwaambukiza watu wa Nairobi na Kilifi,” aliongeza na kufafanua kuwa nafasi ya uongozi au madaraka haviwezi kumlinda yeye dhidi ya matokeo ya mkosa yake.

Jana, Naibu Gavana huyo alifikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria. Mkurugenzi wa Mashtaka aliiomba Mahakama kumhamishia kwenye moja kati ya magereza yenye ulinzi mkali zaidi nchini humo wakati jeshi la polisi likiendelea na upelelezi dhidi yake.

Gereza la Manyani ni gereza la tano kwa ukubwa nchini Kenya na liko kwenye eneo la ‘machakani’ la Tsavo lililoko Kaunti ya Taita Taveta.

Hakimu Mkazi Mwandamizi, Ritah Amwayi alisema kuwa atatoa uamuzi wake Aprili 9, 2020 kuhusu kuendelea kumshikilia au kumpa dhamana. Kwa sasa anaendelea kushikiliwa na polisi chini ya uangalizi wa wataalam wa afya.

Hadi sasa watu 4,277 wamepimwa nchini humo, 158 wamebainika kuwa na virusi vya corona, sita wamepoteza maisha na wanne wamepona.

Rais FIGC akataa kufuta msimu wa Serie A
Fahamu vyakula vya ajabu vinavyoliwa na wachina