Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera Jumanne amemuondolea Makamu wake Saulos Chilima madaraka yote aliyokabidhiwa baada ya kutajwa katika kashfa ya ufisadi kwenye mikataba ya Serikali inayowahusisha Maafisa Wakuu kadhaa.

Hatua ya Rais huyo inafuatia taarifa ya ripoti mpya ya Taasisi ya Kupambana na Rushwa (ACB), ambayo inamchunguza mfanyabiashara kutoka Uingereza na Malawi, Zuneth Sattar kwa tuhuma za rushwa, ulaghai na utakatishaji haramu wa fedha.

Kupitia hotuba yake aliyoitoa kwenye Luninga, Chakwera amesema ameamua kuondoa majukumu yote aliyokabidhiwa kutoka kwa Makamu wake wa Rais, Saulos Chilima.

“Ofisi iligundua kuwa jumla ya maafisa 53 wa umma na maafisa wa zamani wa umma walidaiwa kupokea pesa kutoka kwa Bw Sattar katika muda wa miezi minane kati ya Machi na Oktoba 2021,” amesema Chakwera.

Rais wa Malawi pia alimsimamisha kazi Mkuu wake wa kazi na Mkuu wa polisi wa nchi hiyo na tayari Mawaziri kadhaa wakiwemo na Mawaziri wa zamani wamekamatwa kuhusiana na kesi hiyo.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa Ofisi hiyo iligundua kuwa watu wengine 31 kutoka sekta binafsi, vyombo vya Habari, Mashirika ya kiraia na taaluma ya Sheria huku pia wakipokea pesa kutoka kwa Sattar, na kufanya jumla ya watu 84 wanaoshukiwa kuhusika na kashfa hiyo.

Aidha, Polisi na Wanajeshi wameripotiwa kutoa kandarasi 16 zenye thamani ya dola milioni 150 kwa kampuni tano zinazomilikiwa na Sattar kati ya mwaka 2017 na 2021.

Mapema mwaka 2020 Saulos Chilima, mgombea urais, alishirikiana na Lazarus Chakwera kushinda uchaguzi wa marudio kufuatia udanganyifu katika kura ya kwanza ya mwaka 2019.

Waliotekwa na Boko Haram wapatikana wakiwa na watoto
Mbaroni kwa kucheza muziki Msikitini