Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein ameweka wazi msimamo wa Chama hicho kwamba kitawapitisha kugombea katika nafasi za uongozi wale tu wenye mapenzi ya dhati na moyo wa kukitumikia Chama hicho.

Ametoa msimamo huo wakati akihutubia Wanachama na Wananchi katika ziara yake ya kukagua shughuli za Chama na Serikali katika Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema kuwa Chama kitawapitisha wale wote watakaobainika kufuata vyema taratibu na miongozo mbalimbali ya Chama na wale wasiokuwa na sifa wasipoteze muda kugombea.

“Nasema wazi asiyekitumikia Chama Fomu za kugombea hapewi, asigombee bure, Chama kina maadili yake na Serikali ina maadili yake asiyeweza kufuata maadili aache,”amesema Dkt. Shein

Aidha, ameendelea kutoa tahadhari kwa Viongozi mbalimbali hasa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa na lugha nzuri wakati wa kuchangia hoja mbalimbali ili kuepuka kuichafua Serikali na Chama kwa ujumla.

Hata hivyo amesisitiza kuwa Wajumbe hao hawakatazwi kuihoji Serikali kwa vile ndio wajibu wao wa msingi lakini wanapaswa kuzingatia lugha nzuri wakati wa mijadala.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja, Idrisa Kitwana Mustafa amesema kuwa Wilaya hiyo imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuiwezesha Wilaya kukusanya shilingi Milioni 488 mwaka jana.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheri amesisitiza Wananchi wa Mkoa wa Kusini kujiepusha na Vitendo vya magendo ambavyo vinalikosesha taifa mapato.

 

Mwinyi Zahera afunguka kuhusu Mbao FC
Lugola aagiza iundwe tume ya uchunguzi, 'Haiwezekani mwananchi ateswe na Polisi'