Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amepiga marufuku mizunguko yoyote ya barabara, reli na anga ndani na nje ya jiji la Nairobi katika maeneo yenye watu wengi kuanzia leo, Aprili 6, 2020.

Akilihutubia taifa hilo kutoka Ikulu, amesema kuwa uamuzi huo umelenga katika kupambana na kusambaa kwa virusi vya corona kwenye maeneo mengine ya nchi, kwakuwa asilimia 82 ya visa vilivyoripotiwa nchini humo vimetokea jijini Nairobi.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa nchi, kumekuwa na ongezeko la visa 16 vya wagonjwa wa corona. Hadi sasa kuna visa 158 vilivyorekodiwa nchini humo na vifo sita vinavyotokana na virusi vipya vya corona (covid-19).

Rais Kenyatta pia amepiga marufuku mizunguko na usafiri katika kaunti tatu za nchi hiyo za maeneo ya Pwani ambazo ni Kilifi, Kwale na Mombasa ambapo asilimia 14 ya visa vilivyoongezeka nchini humo vimetokea katika maeneo hayo.

“Marufuku ya mizunguko ndani ya eneo la katikati ya jiji la Nairobi itakuwa ya siku 21 katika kipindi cha awali kuanzia Jumatatu, Aprili 6, 2020 saa moja kamili usiku,” amesema Rais Kenyatta na kuongeza kuwa katika kaunti tatu zilizotajwa itaanza Aprili 8, 2020.

Aliyataja maeneo ya Nairobi ambayo yataathirika kutokana na katazo hilo kuwa ni kaunti ya jiji la Nairobi, sehemu ya Kiambu hadi Daraja la Mto Chania, Thika, Rironi, Ndenderu, Mji wa Kiambu Mjini, sehemu ya Kaunti ya Machakos hadi Mto Athi ikiwa ni pamoja na Kathani.

Pia, eneo la Kaunti ya Kajiado likijumuisha Kitengela, Kiserian, Ongata Rongai na Mji wa Ngong.

Vandenbroeck: Ni mapema sana kufuta ligi
Video: Makonda asema watakaokamatwa uzururaji watasafisha mitaro