Baadhi ya wanasiasa na wachambuzi wa mambo ya kisiasa wamemkosoa Rais John Magufuli kwa kutohudhuria mikutano ya Kimataifa ukiwemo mkutano wa Umoja wa Afrika (AU), uliofanyika Addis Ababa nchini Ethiopia hivi karibuni wakidai kuwa ulikuwa muhimu sana kidiplomasia.

Wameeleza kuwa mkutano huo wa AU uliofanyika siku mbili nchini Ethiopia ulikuwa muhimu sana kwa kuzingatia utamaduni wa mikutano hiyo kuwakaribisha viongozi wapya wa nchi wanachama.

“Kama Mkuu wa nchi, Rais Magufuli alipaswa kuhudhuria mkutano huo ili akutane na viongozi wenzake na kubadilishana nao mawazo. Nadhani hayuko sahihi kwenye hili,” Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholas Mgaya aliliambia gazeti la The Citizen.

“Kwa namna hii, Tanzania inapoteza mengi, taswira yetu inafifia kwenye ngazi za kimataifa. Kiongozi wetu anapaswa kuona umuhimu wa kuhudhuria kwenye vikao kama hivyo vya kimataifa vya ngazi za juu,” aliongeza Mgaya.

Naye mhadhiri Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco) ambaye ni mtaalam wa masuala ya kisiasa, Profesa Gaudence Mpangala aliunga mkono na kueleza kuwa mkutano huo ulikuwa na umuhimu sana kwa Rais Magufuli kuhudhuria akiwa na ujumbe wa viongozi wachache.

“Kama Rais Magufuli amepanga kupunguza gharama, angeenda na watumishi wachache. Lakini mkutano huo ulikuwa muhimu sana kwake na Taifa,” alisema Profesa Mpangala.

Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Ikulu, Gerson Msigwa alieleza kuwa Rais Magufuli alimtuma Makamo wa Rais, Bi. Samia Suluhu kuiwakilisha nchi kwa kuwa alikuwa na majukumu mengine nchini. Kwahiyo nchi iliwakilishwa vyema kwenye mkutano huo.

“Kama Rais hakuhudhuria ina maana alikuwa na majukumu mengine. Lakini aliwakilishwa na Makamo wa Rais. Kwahiyo kila kinachohusu Tanzania kitafanyiwa kazi ipasavyo,” Msigwa aliliambia gazeti la The Citizen.

Aidha alisema kuwa bado kuna mikutano mingi ya Umoja wa Afrika mbeleni ambayo Rais Magufuli atahudhuria.

 

 

Majipu, Mbwa na Askari Bungeni vyamgusa Askofu Mkuu KKKT
Mwanasiasa apendekeza wakimbizi wapigwe risasi