Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli leo emekutana na Dkt. Wilbroad Slaa, Ikulu jijini Dar es Salaam ikiwa ni mara ya kwanza tangu alipomteua kuwa Balozi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, Dkt. Slaa amempongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya na kwamba ametekeleza mambo mengi ambayo yalipigiwa kelele kwa takribani miaka 20 iliyopita.

“Kwakweli nimepata faraja kwa sababu Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza hatua kwa hatua karibu yote tuliyokuwa tunayapigania kwa miaka takribani 20 huko nyuma. Mimi nilikuwa napiga kelele kwa sababu nilikuwa naona kuna upungufu,” taarifa hiyo inamnukuu Dkt. Slaa.

Naye Rais Magufuli amemsifia Dkt. Slaa kuwa ni Mtanzania mzalendo mwenye moyo safi ambaye anaamini atatekeleza majukumu yake vizuri kama Balozi katika nchi atakayopangiwa.

“Dkt. Slaa alinijulisha kuwa anakuja na akaomba akija aweze kuniona, nikampangia leo. Tumezungumza mambo mengi na ameniahidi kuwa atakwenda kufanya kazi yake vizuri kwenye nchi atakayokwenda kuwa Balozi,” alisema Rais Magufuli kwa mujibu wa taarifa hiyo.

Dkt. Slaa ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo na kugombea nafasi ya Urais, mwaka 2015 alitangaza kuachana na masuala ya siasa baada ya chama hicho kumkaribisha waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na kumpa nafasi ya kugombea urais kupitia umoja wa vyama vitano vya upinzani ulioitwa Ukawa.

Rais Magufuli alimteua kuwa Balozi na anasubiri kumpangia nchi atakayokwenda kuiwakilisha Tanzania.

Video: Meya wa Jiji atoa ufafanuzi kukamatwa gari lake
Nabii Tito aanza kushughulikiwa