Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli, amempa zawadi ya kihistoria Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama aliyekuwa nchini hadi jana.

Obama aliingia nchini kwa ajili ya kutembelea vivutio vya utalii akiwa na familia yake, na alitalii katika mbuga ya wanyama ya Serengeti mkoani Mara kabla ya kuondoka jana kuelekea nchini Kenya.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga alimpokea na kufanya mazungumzo na Obama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), kabla ya kuondoka nchini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga akimpokea Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, KIA

Balozi Mahiga alisema kuwa Rais Magufuli amempa Obama zawadi ya picha maalum ya tukio la nyumbu wanaohama katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Tukio hilo liliingia kwenye historia ya utalii duniani kama tukio la kipekee.

Akieleza kwanini uwepo wa Obama nchini haukutangazwa, Balozi Mahiga alisema kuwa ilitokana na sababu ya msingi kuwa ilikuwa ziara yake binafsi.

“Alikuja kutembelea hifadhi ya Serengeti kwa safari binafsi hivyo ni lazima tuheshimu hilo,” alisema Balozi Mahiga.

Ujio wa Obama kwenye hifadhi hizo umemvuta pia Rais wa Uswis, Alain Berset pamoja na familia yake ambao wapo nchini kwa ajili ya kuangalia vivutio vya utalii.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Bodi ya Utalii nchini, kwa mwaka jana watalii kutoka Marekani ya Kaskazini walikuwa wanaongoza kwa ujumla ikiwa ni watalii 107,361 waliowasili. Kati ya hao, Marekani pekee ilikuwa na asilimia 81 ya raia wake waliokuja kutalii, sawa na watalii 87,238.

Hali hii inatokana na ubora wa hifadhi za vivutio vya utalii nchini pamoja na jitihada za kutangaza vivutio hivyo.

Adil Rami ajiengua Les Bleus (The Blues)
LIVE: Sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi chuo cha uongozi cha Julius Nyerere