Rais John Magufuli leo amemteua Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Semistocles Kaijage kuwa Mwenyekiti mpya wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC).

Jaji Kaijage anachukua nafasi ya Jaji (Mstaafu), Damian Lubuva ambaye alimaliza muda wake tangu Desemba 19 mwaka huu. Kaijage ataendesha mashua ya NEC kwa kipindi cha miaka mitano.

Taarifa ya uteuzi huo iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi imeeleza kuwa Rais Magufuli pia amemteua Jaji (mstaafu) Hamid Mahamoud Hamid kuendelea kuwa Makamu Mwenyekiti wa NEC kwa kipindi cha miaka mitano.

Kama ilivyokuwa kwa Jaji Lubuva, Jaji Hamid alikuwa amemaliza muda wake wa uteuzi wa mwanzo katika nafasi hiyo tangu Desemba 19 mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemteua Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Jaji Harold Nsekela kuwa Kamishna wa Maadili katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Desemba 20 mwaka huu, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Salome Kaganda aliyestaafu mwezi huu.

Rais Magufuli pia amewateua majaji wanne wa Mahakama Kuu kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufaa ambao wataapishwa rasmi kesho.

Majaji walioteuliwa ni Jaji Dk. Gerald Ndika, Jaji Jackobs Mwambegele, Jaji Rehema Mkuye na Jaji Sivangilwe Mwangesi.

Video: Tamko la Jeshi la Polisi nchini kuelekea X-Mass na mwaka mpya
Video: Kamanda Mpinga asitisha utendaji wa CHAKUA mikoani