Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli leo ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) , Dk Edward Hoseah.

Taarifa ya utenguzi huo imetolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue na kueleza kuwa Rais Magufuli amechukua hatua hiyo kutokana na kutoridhishwa na utendaji na mwenendo wa Taasisi hiyo katika kuzuia na kupambana na rushwa chini ya Dk. Hoseah.

Ameeleza kuwa Rais Magufuli ameonesha kutoridhika na namna ambavyo Takukuru imeshindwa kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya rushwa hususan katika eneo la Bandari ambapo kiasi kikubwa cha fedha za umma kimepotea kwa ubadhirifu na rushwa.

“Rais amesikitishwa na taarifa za kuwepo vitendo vya rushwa katika eneo hilo kwa muda mrefu, lakini kasi ya Takukuru kuchukua hatua haiendani na Kasi anayotaka, “alisema Balozi Sefue.

Aidha, Balozi Sefue ameeleza kuwa rais Magufuli amemteua aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowoka Kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo.

Aliyekuwa Mkurugenzi Manispaa ya Kinondoni Asimamishwa Kazi
Mkutano Mkuu Wa TFF Waahirishwa