Rais John Magufuli jana aliwashukia viongozi wa siasa wanaotoa kauli za kuwatetea watu walioko mahabusu, kauli ambayo hivi karibuni ilimtia matatani waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na kuhojiwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).

Akihutubia wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuboresha Bandari ya Dar es Salaam, Rais Magufuli aliwakemea viongozi wenye kauli kama hizo akiwataka kujifunza kufunga midomo yao.

“Unakuta kiongozi wa siasa anasema watu fulani waondolewe mahabusu. Hajui kuna wengine walikaa Gwantanano Bay miaka na miaka? Sitaki kuona suala hili linaendelea, tuweke uzalendo mbele,” alisema Rais Magufuli.

“Unaweza ukaona huyo anayetetea walio mahabusu naye anahusika kwa namna moja au nyingine. Wajifunze kufunga midomo yao wakati Serikali inafanya kazi yake,” aliongeza.

Aidha, alilitaka Jeshi la Polisi kufanya kazi yake bila kuangalia mtu anayehusika, “awe ana mwendo wa haraka, awe ana mwendo wa polepole, fanyeni kazi yenu.”

Lowassa alitoa kauli ya kumuomba Rais Magufuli kuwaachia mashehe wa Jumuiya ya Uamsho waliokamatwa mwaka 2012, wakati wa kushiriki futari iliyoandaliwa na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara akishirikiana na madiwani wa Chadema jijini Dar es Salaam.

Mwanasiasa huyo aliyewania kiti cha urais katika uchaguzi wa mwaka 2015, alisema kuwa mashehe hao wamekaa mahabusu zaidi ya miaka minne na kwamba mtu pekee anayeweza kuwatoa gerezani kama sio mahakama ni Rais Magufuli.

Hata hivyo, Lowassa aliendelea kushikilia msimamo wake hata baada ya kuhojiwa na ofisi ya DCI, akidai kuwa anaamini hakufanya kosa kwenye kauli yake na ataisimamia. Anatarajia kurejea tena kwenye ofisi hiyo kwa ajili ya mahojiano katikati ya mwezi huu.

Video: JPM atoa onyo kwa wanasiasa, Bandari Dar sasa habari nyingine
Magazeti ya Tanzania leo Julai 3, 2017