Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli leo Februari 25, 2021 amewataka Wananchi pamoja na waandishi wa habari kutanguliza maslahi ya Taifa.

Ameyasema hayo wakati akihutubia wananchi waliojitokeza katika Uwanja wa Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam baada ya kuweka jiwe la msingi katika Soko Kuu la Kisutu na kuzindua Jengo la Jitegemee (Ofisi za Africa Media Group Limited) lenye vituo vya Channel Ten, Magic FM, Channel Ten Plus na Classic FM.

Akiwa kwenye Studio mpya za Channel Ten Rais Magufuli alichagua kupigiwa wimbo wa Baba ulioimbwa na Stamina akishirikiana na Msanii Mkongwe nchini Profesa Jay na One Six na kusema kuwa wimbo huo una ujumbe.

Aidha Rais Magufuli amesema si wanahabari pekee wenye uwezo wa kuchafua sifa ya nchi bali hata wananchi wengine wanaweza kufanya hayo kwa kutumia mitandao ya kijamii, huku madhara ya tabia hiyo yakiwa ni makubwa kwa Taifa.

Ameeleza kuwa kwa miaka mitano, serikali imeimarisha haki na wajibu wa vyombo vya habari ambapo usajili wa vyombo mbalimbali umeongezeka kufikia vituo vya redio 193, vituo vya TV 46, redio za mitandaoni 23 pamoja na magazeti na majarida 247.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amemshukuru Rais Magufuli kwa kuzindua kituo hicho cha habari na kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Wizara hiyo.

Bashungwa ametumia jukwaa hilo kuwashawishi wawekezaji wengine na Chama cha Mapinduzi ambacho ndiyo mmiliki wa Africa Media Group Limited kuwekeza pia kwenye sekta ya michezo kwani kuna viwanja vingi katika maeneo mbalimbali nchini.

Serikali na kasi mpya kukuza teknolojia
Halima Mdee aachiwa huru