Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ameusifia uamuzi alioufanya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kwa uamuzi aliouchukua wa kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana.

Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha

Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha

Akihutubia leo mamia wa wananchi wa Pemba katika ziara yake visiwani humo, Rais Magufuli amesema kuwa Jecha alichukua uamuzi sahihi kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar.

Aidha, alimshauri Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kumpa tuzo ya heshima Mwenyekiti huyo wa ZEC.

“Nampongeza sana Jecha kwa kazi nzuri aliyofanya kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, na kwa kweli Dk. Shein kama tuzo zako utakazotoa, naomba usimsahau kumpa na Jecha,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amewatahadharisha wale wote wanaotaka kuvunja amani ya nchi kuacha mara moja kwani watashughulikiwa.

Aliyataka majeshi ya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua bila huruma wale wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya kuchoma karafuu na mashamba ya wenzao.

Zanzibar imekumbwa na uhasama wa kisiasa kati ya CCM na CUF kutokana na kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 na kufanyika kwa uchaguzi wa marudio wa Machi 20 mwaka huu.

CUF walisusia uchaguzi wa marudio na kupelekea CCM kupata ushindi mnono wa asilimia zaidi ya 90.

Credit: Mwanahalisi Online

Magufuli awataka CUF kuacha ndoto za mchana
Katibu Mkuu Wizara Ya Ujenzi Uchukuzi Na Mawasiliano Atoa Neno Kwa Vyuo