Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli ametoa siku saba kwa Wakuu wa Mikoa inayozalisha dhahabu nchini kushirikiana na Wizara ya Madini katika kufungua masoko ya madini ikiwemo dhahabu ili kuifanya sekta ya madini kuweza kuleta tija ya kiuchumi kwa Watanzania wote hususani wachimbaji wadogo.

Ametoa agizo hilo mkoani Mbeya wakati wa hafla ya uzinduzi na uwekaji wa jiwe la msingi la barabara ya Mbeya-Lwanjilo-Chunya-Makongolosi yenye urefu wa Kilometa 111, ambapo amesema kuwa Serikali anayoiongoza kamwe haitokubali kuona wachimbaji wadogo wakiendelea kuteseka nchini.

Amesema kuwa tangu mwaka 2017, Serikali imepitisha Sheria Bungeni inayotoa maelekezo kuhusu usimamizi wa sekta ya madini nchini na hivyo anashangazwa na baadhi ya Viongozi wake hususani Wakuu wa Mikoa inayozalisha dhahabu kusuasua katika kusimamia maelekezo ya maelekezo yake aliyoyatoa katika siku za nyuma.

Aidha, ameongeza kuwa Serikali pia imefuta kodi mbalimbali za madini na kuendelea kuwahamasisha wachimbaji wadogo kupeleka dhahabu zao katika masoko hayo, lakini hadi sasa baadhi ya Wakuu wa Mikoa wameshindwa kujenga masoko hayo, pamoja na faida mbalimbali zinazopatikana katika masoko hayo ikiwemo kuepusha dhuluma kwa wachimbaji, kupata dhahabu yenye ushindani pamoja na kuzuia upotevu wa kodi ya Serikali.

Pia amesema kuwa katika mkutano wake alioufanya hivi karibuni na Viongozi wa Wizara ya Madini na Wakuu wa Mikoa ya Tanzania Bara inayozalisha Dhababu, alitoa maelekezo ya kufungua masoko ya madini katika maeneo yao, ingawa ni Mkoa wa Geita pekee uliyotekeleza maelekezo hayo wakati ujenzi huo hauhitaji nyumba au eneo kubwa.

“Kama Mkoa wa Geita, umeweza kuwa na Kituo cha soko la kuuzia madini, nashangazwa kwanini Wakuu wengine wa Mikoa wanashindwa kutekeleza maelekezo hayo, hivyo hili ni agizo kwa Wakuu wa Mikoa ya Katavi, Singida na Arusha kuhakikisha kuwa watatekeleza maagizo haya,”amesema Rais Magufuli.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, amesema kuwa suala la kujiletea maendeleo kwa Watanzania linacheleweshwa na baadhi ya Viongozi, Watendaji Serikali kwani wananchi hususani wachimbaji wadogo wa madini wamekuwa na juhudi kubwa za kujiletea maendeleo yao lakini wamekuwa wakikatishwa tamaa pamoja na juhudi kubwa wanazozionyesha katika kuchimba dhahabu.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Dotto Biteko amesema tangu kutungwa kwa Sheria ya Madini mwaka 2017, Serikali imeweza kuokoa kiasi kikubwa cha madini kutoroshwa nje ya nchi, ambapo katika Wilaya ya Chunya ambayo ni Wilaya ya pili kwa uzalishaji wa dhahabu Serikali imeweza kutoa jumla ya kilo 30 zilizokuwa zikitoroshwa nje ya nchi kutokana na kukosekana kwa mtambo wa kuchenjulia madini.

 

Waziri Mkuu awaaga Watalii 1000 kutoka Israel
Peter wa P-Square ajibu kuhusu kuchepuka na Zari, Zari amwagia sifa