Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa hakuna uchaguzi mwingine katika kuhakikisha Afrika inaondokana na unyonge zaidi ya kuungana katika mapambano ya kiuchumi.

Ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam wakati akiwa na mgeni wake, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa wakati wa jukwaa la biashara kati ya wafanyabiashara kutoka nchi za Afrika Kusini na Tanzania katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) ambapo amesisitiza kuwa hakuna kinachoweza kuzuia Afrika kuwa na maendeleo.

Amesema kuwa zaidia ya asilimia 70 ya uzalishaji katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) bidhaa zinakwenda Afrika Kusini, ikiwemo mbogamboga na matunda, nafaka, vinywaji, mpira na huduma za usafiri.

Amebainisha kuwa, Afrika Kusini ni nchi ya pili kwa uwekezaji nchini ambapo kwa mwaka jana 2018 mauzo katika biashara baina ya Tanzania na Afrika Kusini yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 5.3.

“Sekta ya viwanda inazidi kuongeza urafiki huu, hata hivyo uzalisihaji wetu katika taifa la Tanzania bado uko chini, kama taifa tunaamini tunahuisha uwekezaji wa viwanda ambavyo vinaongeza thamani katika bidhaa zetu ambazo zinasafirishwa zikiwa ghafi na kupunguza bidhaa kutoka Ulaya,” amesema Rais Magufuli

“Afrika Kusini ni ya 13 kwa uwekezaji nchini, takwimu zinaonyesha uhusiano wetu katika uchumi ni mkubwa, maendeleo haya yanaonyesha urafiki wetu wa kibiashara, kiuchumi, kijamii na kisiasa unaimarisha uwekezaji huu, ”amesisitiza

Aidha, Rais Magufuli amekuwa mkali kwa watu wanaosambaza uongo kuwa Tanzania si sehemu salama kwa wawekezaji, ambapo amesema kuwa huo ni uongo unapaswa kupuuzwa kwani Tanzania inasifika kwa amani na utulivu wa kisiasa.

Kwa upande wake, Rais Cyril Ramaphosa amesema kuwa Tanzania na Afrika Kusini zina urafiki wa miaka mingi, hakuna maneno ya kueleza kwa namna ilivyowasaidia wakati wa kuhangaika, wakati wa kipindi kigumu.

“Mlitufunza, mlituunga mkono kwa njia nyingi na kutusaidia kiasi kikubwa, tunashukuru kwa dhati. hii ndio sababu muunganiko wetu si wa kihistoria tu bali wa damu, kujitoa kwenu muhanga na kutuunga mkono katika mapambano ndio maana leo Afrika Kusini imekuwa huru,”amesema Ramaphosa

”Jamii ya wafanyabiashara Afrika Kusini wanafikia asilimia 70, maana yake fursa hii hatutaiacha, tuna kampuni zaidi ya 208 hapa Tanzania ambapo kuna waajiriwa zaidi ya 21,000,”amesisitiza

 

Skimu 100 za umwagiliaji zanufaika na mafunzo nchini
LIVE IKULU: Rais Magufuli akizungumza na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa