Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewataka watumishi wa umma kuachana na utamaduni wa kila kitu wanachokifanya kudai ni maagizo kutoka juu.

Amesema hayo wakati akitoa salamu za mwaka mpya ambapo amesema kuwa utamaduni huo ni ugonjwa ambao umeanza kuwapata watumishi wa umma ambapo kila wanalolifanya hata kama ni kwa mujibu wa sheria hawataki kujiamini, na wanasema hili ni maagizo kutoka juu.

Rais Magufuli amesema hayo kutokana na watendaji mbalimbali Serikalini kutumia neno hilo katika utekelezaji wa majukumu yao, hasa masuala yanayowahusu wananchi.

“Na mara nyingi maagizo yanakuwa hayapo, bali ni utekelezaji wa wajibu wa sheria, wajiamini na wasiwaonee watu lakini watimize wajibu wao,” alisema.

Rais Magufuli amesema mwaka huu utakuwa wa mafanikio zaidi kiuchumi na kuwataka Watanzania kudumisha amani, upendo, umoja na mshikamano.

“Ujumbe wangu kwa watumishi wa umma, ni kama nilivyotoa ujumbe kwa Watanzania wengine, wachape kazi, wajiamini,” aliongeza.

Pia, amewataka viongozi mbalimbali, wakulima, wafanyabiashara, wavuvi na wafugaji kuongeza juhudi za uzalishaji mali kupiga vita rushwa, wizi, ufisadi na ubadhirifu.

Aidha, Rais Magufuli amezungumzia mwaka 2018 kuwa ulikuwa mwaka wa mafanikio na mambo mengi yalifanyika katika uchumi wa nchi ambayo Watanzania wameyashuhudia katika maeneo yao na mengine.

“Tuipende Tanzania yetu, amani yetu na umoja wetu na tuendelee kumtanguliza Mungu kila mmoja katika imani yake. Nina imani uchumi kwa mwaka 2019 utapanda zaidi, tulinde amani tuitangulize Tanzania kwanza na kuchapa kazi.”

Somalia yamtimua Balozi wa UN aliyewalima barua
Video: Panya Road watikisa Dar mwaka mpya, JPM apiga marufuku maagizo kutoka juu