Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanania, Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa katika hali isiyokuwa ya kawaida baadhi ya abiria wamekuwa wakikosa tiketi kwa kuambiwa ndege imejaa ila wanapoingia ndani hakuna watu huku baadhi ya tiketi zikiwa za watendaji wa Serikali ambao hawasafiri.

Rais Magufuli amesema hayo leo Desemba 23, 2018 wakati akipokea ndege mpya ya Airbus 220-300 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam ambapo amesema viongozi hao wa Serikali waliokatiwa tiketi ili wasafiri na ndege za Shirika la ATCL na kukaidi watakatwa pesa hizo katika mishahara yao..

“Mtumishi amekatiwa tiketi na Serikali lakini hasafiri na kufanya ndege iende tupu, nimeshamwambia mtendaji mkuu aniletee orodha ya watendaji ambao hawakusafiri tuwakate hizo hela kwenye mishahara yao,” amesema Rais Magufuli.

Amesema watumishi hao wajiandae kurudisha fedha hizo kutoka mifukoni mwao ili iwe fundisho kwa watumishi wengine wanaotumia fedha za Serikali vibaya.

“Nimeambiwa wanakadiriwa kuwa 100 kwa hiyo nina uhakika kufika wiki ijayo nitapata majina yao, mawaziri, wabunge ambao walikaa hadi saa ya mwisho ndege ikaenda tupu na hela za Serikali zikaenda,” ameongeza Rais Magufuli huku akisema tena anafikiri kesho Jumatatu yatamfikia.

“Niwaombe tu watendaji kama kuna tiketi ambayo haukuitumia leta tu hela mara moja ili mambo yaishe lakini ni matumaini yangu sasa katika suala hili la tiketi ATCL mtajipanga vizuri,” amesema Magufuli.

Ndege hiyo iliyopokelewa leo na Rais Magufuli ina uwezo wa kubeba abiria 132 ambapo 12 kati yao ni wa daraja la biashara na 120 ni daraja la kawaida.


Live: Rais Magufuli akipokea ndege mpya ya Tanzania

Simba yaleta raha, yaizamisha Nkana FC Uwanja wa Taifa
Ndugai: Tuunge mkono juhudi za Rais Magufuli, 'Tulikuwa tunachekwa hadi na nchi ndogo'