Bila shaka Kasi ya rais John Magufuli imeigusa kwa namna chanya asilimia 98 ya watanzania wote ambao wamekuwa wakilalamikia ubadhirifu na kutochukuliwa hatua stahiki watendaji ambao wanaonekana kutowajibika ipasavyo au uwajibikaji wao hautoi matunda yanayotarajiwa.

Nimeacha asilimia mbili za watanzania ambao huenda kwa namna moja ama nyingine walikuwa wanafaidika zaidi na ubadhirifu ama uzembe wa baadhi ya watendaji hivyo ni waathirika wa kasi ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dk. John Magufuli.

Tumekuwa tukisikia wapinzani wakidai kuwa rais Magufuli anatekeleza ilani ya vyama vyao na sio ilani ya CCM. Kiongozi Mkuu wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe aliwahi kusema kuwa hotuba ya rais Magufuli imebeba asilimia 60 ya ilani ya chama chake ambayo walimkabidhi siku aliyopewa cheti cha ushindi.

Naye mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema rais Magufuli anatekeleza kile ambacho wapinzani walikuwa wanakipigia kelele huku wakipingwa na CCM. Madai ambayo CCM iliyakanusha vikali.

Hata hivyo, aliyekuwa katibu mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa ni mmoja kati ya wanasiasa wakongwe waliokuwa wapinzani ambao walianza kuzikubali sera za Dk. Magufuli wakati wa kampeni na kutangaza dhahiri kumuunga mkono kwa madai kuwa alikuwa na nia ya dhati ya kulitumikia Taifa na kuwatetea wanyonge.

Moja kati ya hoja za Dk. Magufuli zilizomkuna Dk. Slaa ni suala la kupambana na rushwa na ufisadi nchini, sera ambazo Dk. Slaa akiwa ndani ya Chadema alikuwa akizihubiri kwa nguvu na kupata umaarufu mkubwa.

Baada ya kujiuzulu nafasi yake ya ukatibu mkuu wa Chadema na kujitokeza hadharani kuonesha namna anavyopinga suala ya Edward Lowassa kujiunga na chama hicho na kupewa nafasi ya kugombea urais, Dk. Slaa alizungumza moja kwa moja kupitia runinga na kueleza baadhi ya mambo ambayo aliyaita uozo uliotokana na sakaka la Richmond.

Dk. Slaa alionesha namna ambavyo Takukuru walishindwa kutekeleza majukumu yake na kueleza kuwa taasisi hiyo inaviashiria vya rushwa hivyo inahitaji taasisi nyingine yenye majukumu kama hayo kuichunguza.

“Takukuru nayo inahitaji Takukuru nyingine ya kuichukunguza,” alisema Dk. Slaa wakati akizungumza moja kwa moja na vyombo vya habari kutoka katika hotel ya Serena Jijini Dar es Salaam wakati kampeni za urais zikiendelea.

Ni kama sikio la Dk. Magufuli liliisikia sauti ya Dk. Slaa na kuifanyia kazi ama walikuwa wote wanamtazamo unaofanana kuhusu utendaji wa Takukuru.

Siku chache baada ya kuingia madarakani, Rais John Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah na kueleza kuwa hakuridhishwa na utendaji wa taasisi hiyo katika kutekeleza majukumu yake.

Kutokana na uamuzi huo wa rais Magufuli, ni dhahiri kuwa Dk. Slaa ambaye alikuwa kiongozi wa vita dhidi ya ufisadi na rushwa akiwa kama mpinzani, amefurahishwa na kile anachokifanya Dk. Magufuli hivyo wawili hao walikuwa na mtazamo mmoja.

Wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa nchini wanaeleza kuwa kasi ya Dk. Magufuli ikiendelea vizuri hususani katika kupambana na rushwa na ufisadi, itaendelea kufifisha upinzani nchini na huenda asipate upinzani mkubwa katika uchaguzi wa mwaka 2020. Hii ni kwa sababu hoja ya kupambana na rushwa na ufisadi iliyokuwa imebebwa na Chadema hivi sasa inaonekana kufanyiwa kazi kwa vitendo na serikali ya awamu ya tano.

Kiasi watakacholipwa wasanii kwa kucheza nyimbo zao redioni na kwenye TV chawekwa wazi
Afisa Wa Jeshi la Polisi Ajinyonga