Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amesema ujenzi wa ukuta katika mgodi wa Mererani umesaidia madini ya Tanzanite kutotoroshwa nje ya nchi.

Magufuli ametoa kauli hiyo mjini Dodoma mapema hii leo, wakati akizungumza na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya kuchukua fomu za kugombea nafasi ya Urais kwa awamu ya pili katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Rais Magufuli amesema matokeo ya kujengwa kwa ukuta huo yameanza kuonekana kwa kuwanufaisha wachimbaji wazawa pamoja na kuinufaisha serikali kupitia sekta ya madini.

“Tumechezewa sana kwenye madini, wapo watu walizungumza hadharani kwamba tutashughulikiwa na tutanyooshwa, nilisimama pamoja na wana CCM wenzangu kwamba ni bora kufa ukaifia nchi yako, ndiyo maana leo mnaona mpaka Mmasai Laizer anachimba anapata Jiwe la Tanzanite,” amesema.

“Zamani hawakuyaona mbona, yalienda wapi? Wana-CCM katika kufikiria haya tukiondoka wale wenye rangi nyingine ambazo hazifanani na Kijani watakuja kweli kuyafanya haya?” Rais Magufuli alihoji.

Alihoji pia, kwa jinsi gani watu waliokuwa wanashirikiana na mabeberu kuiibia Tanzania madini, leo wanaweza kugeuka kuwa watu wema wa kuwasaidia Watanzania.

Rais Magufuli awashukuru wapinzani kwa kumpigia kampeni
Watalii waendelea kumiminika Tanzania, ndege kubwa zatua na mamia