Rais wa  Shirikisho la soka nchini TFF, Jamal Malinzi, amemtumia salamu za rambirambi kwa Mwenyekiti wa Young Africans Sports Club, Yussuf Manji kutokana na kifo cha Makamu Mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Isaac Shekiondo ‘Clinton’.

Shekiondo aliyefariki dunia juzi Novemba 20, mwaka huu kwenye Hospitali ya Amana, Ilala jijini Dar es Salaam, alikuwa Makamu Mwenyekiti katika Kamati ya Muda ya Young Africans chini ya Mwenyekiti Tarimba Abbas na enzi zake Shekiondo anakumbukwa kutokana na ukarimu wake na uwajibikaji mzuri katika klabu.

Katika salamu hizo, Rais Malinzi amesema amepokea kwa masikitiko kifo cha Shekiondo kwa kuwa anafahamu vema utendaji wa Shekiondo wakati huo akiwa Kiongozi wa Young Africans Sports Club. Ni mtu wa soka ambaye amekuwa kwenye tasnia hii kwa muda mrefu wa maisha yake.

Kadhalika Rais Malinzi alituma salamu hizo kwa familia ya marehemu Shekiondo, ndugu, jamaa na marafiki ambayo kwa muda walikuwa wakimuuguza mpendwa wao na hivyo kutokana na kifo hicho, amewataka kuwa watulivu kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya mpendwa wao.

Msiba wa marehemu Shekiondo ulikuwa nyumbani kwake, Ilala  Mchikichini, Dar es Salaam ambapo leo Novemba 22, mwili wake umeagwa katika Kanisa la KKKT Lutheran, Temeke Wailes kabla ya kusafirishwa kwenda Korogwe kwa Shemsi mkoani Tanga kwa mazishi.

Bwana ametoa, bwana ametwaa. Mungu ampumzishe kwa amani marehemu Shekiondo.

Shaka: Ukiona unanyanyaswa ndani ya ccm, milango iko wazi
Hugo Lloris: Ninaheshimu Mkataba Wangu