Aliyekuwa mgombea urais wa Uganda katika uchaguzi uliopita, Amama Mbabazi amemshtaki mahakamani Rais Yoweri Museveni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akipinga matokeo ya uchaguzi huo.

Mbabazi amewasilisha shauri la kupinga matokeo hayo yaliyompa nafasi ya tatu akidai kuwa haukuwa huru na haki na kwamba ulijaa mizengwe.

“Kuna sehemu hakukuwa na ufikishwaji kwa wakati wa vifaa vya kupigia kura. Upigaji kura haukuanza muda uliotangazwa ambao ni saa moja asubuhi, na sehemu nyingine kura zilianza kupigwa saa saba au saa kumi jioni. Kuna sehemu walianza kupiga kura saa mbili usiku na kumaliza saa moja asubuhi,” Mwanasheria wa Mbabazi aliiambia BBC.

Endapo Rais Museveni atathibitishia mahakama kupata nakala za shauri hilo, kesi hiyo inaweza kuanza kusikilizwa mapema wiki ijayo.

Wakati huohuo, aliyekuwa mpinzani mkuu wa Museveni katika uchaguzi huo, Dk. Kizza Besigye ameshindwa kuwasilisha mashtaka yake ya kupinga uchaguzi huo mahakamani kwa kile kilichoelezwa na kiongozi wa chama cha FDC kuwa kilitokana na ufinyu wa muda wa kufungua shitaka hilo kutokana na misukosuko ya kukamatwa kwa mgombea huyo kulikowapotezea muda.

Kiongozi wa chama cha FDC cha Kizza Besigye, Meja Mstaafu Mugisha Muntu alieleza kuwa wameshindwa kuendana na muda wa kufungua shitaka kisheria.

“Alikuwa gerezani mara tisa, hakuweza kukutana na lawyers wake [wanasheria wake] na hakuweza kukutana na wakuu wa chama. Kwahiyo ikatuletea matatizo makubwa na kushindwa kuweka hiyo petition,” alisema Jenerali Mstaafu Muntu.

 

Naibu Katibu Mkuu wa CUF aeleza alichoambiwa akiwa mikononi mwa polisi
Korea Kaskazini kufanya shambulizi la bomu la Nuclear