Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka watanzania vijana kuhakikisha wanakula mlo kamili ili kujiongezea nguvu na Afya ya kuweza kuzalisha watoto na kuongeza Jamii.

Rais ameyasema hayo aliposhiriki hafla ya utiaji saini Mkataba wa Usimamiaji wa Shughuli za Lishe Septemba 30, 2022 jijini Dodoma.

Amesema kuna athari kubwa ya lishe duniani na utapiamlo, na ulaji mbovu ambao hauwasumbui watoto tu bali mpaka wanaume ambao sapo kwenye Umri wa kuongeza familia wanapokosa mlo mzuri wanashindwa kufanikisha jukumu hilo.

Rais Samia amesema ili kulinusuru taifa na madhara hayo ya lishe duni, watafiti wahakikishe wanatoa majibu kamili juu ya sababu zinazosababisha vijana washindwe kuzalisha.

“Tuangalie Ulimwengu wetu sasahivi, mama mjamzito tunamuhangaikia, watoto hawawezi kujitunza tunawahangaikia, Sasa Tuje kwa hawa wa Umri balehe, Kwanini watoto wetu wakifika wakati wa kuongeza familia wanahangaika, mara supu ya pweza, mara udongo wa Kongo sijui, tuna tatizo na mnalijua mnalificha watafiti fanyeni utafiti, lakini tatizo lipo kwenye Lishe” amesema Rais Samia.

Rais Samia ameongeza kuwa “Nasema haya kwa sababu tukiacha yakaenda hivi, tunakwenda kuzalisha taifa goigoi, tunazalisha taifa lenye watu na si rasilimali watu, watakua mzigo kwa Jamii, tutafika mahali hatumjui mke nani na mme nani,”

Aidha Rais Samia amemuelekeza Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kusitisha ujengaji wa vituo vya afya vya kata vipya na badala yake, Wizara ijielekeze kukamilisha Zahanati ambazo zimeanza kujengwa na kuhakikisha vituo vya afya vyote vinaimarishwa na kupata huduma bora pamoja na nyumba za wahudumu.

Rais Samia awakanya wanaosubiri mkeka
Mambo matatu yaliyomuondoa Mzungu Simba SC