Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amekamilisha siku 100 tangu alipoapishwa kushika nafasi hiyo. Kishindo chake kimekuwa kizito na gumzo ndani na nje ya mipaka ya nchi, hasa akiweka historia ya kuwa Rais wa kwanza mwanamke nchini.

Watanzania wamekuwa na maoni mbalimbali kuhusu utawala wa Rais Samia, wengi wakizungumzia hatua mbalimbali zilizowahi kuchukuliwa ndani ya kipindi hicho kifupi, hali iliyowafanya kumuita ‘game changer’, yaani mbadilisha mchezo.

Haki za binadamu:

Fatuma Karume, aliyekuwa Rais wa Tanzania Law Society na mmoja kati ya watu wenye ushawishi wenye mlengo wa kisiasa kwenye mtandao wa Twitter, amezimulika kuwa zilikuwa siku 100 za ‘haki za watu’.

Jumanne Mei 18, 2021 wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha ushonaji, Bohari Kuu ya Jeshi la Polisi, Kurasini jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema Takukuru imefuta kesi 147 ambazo watu walikuwa wamebambikizwa.

Rais Samia aliagiza kuwa kesi za kubambikiwa au zile ambazo Serikali inaona hazina mlengo wenye mantiki ni lazima zifutwe kwani zinaichafua Serikali.

“Takukuru wamefuta kesi 147 ambazo walibambikizia watu,” alisema Rais Samia na kuwataka Polisi pia kufuata nyayo hizo.

Siku chache baadaye, tumeona taarifa za kufutwa kwa mashtaka dhidi ya watu mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na yale mashtaka dhidi ya Masheikh 36 wa UAMSHO waliokaa jela takribani miaka nane wakikabiliwa na mashtaka ya ugaidi.

Rais Samia pia alikita kishindo chake baada ya kumsimamisha aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na baadaye akaingia mikononi mwa vyombo vya dola. Sabaya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya anayedaiwa kuwa hakuwa anakamatika, hivi sasa ameshapandishwa mahakamani na mashtaka dhidi yake yanaendelea kufanyiwa kazi.

Ni katika kipindi cha siku 100 za Samia Suluhu Hassan Ikulu, wateule wake wamepigwa onyo kali la ‘kutopandisha mabega’. Amewataka wateule wake ambao ni wakuu wa wilaya na wakuu mikoa kuhakikisha wanawatumikia wananchi, na sio wanawatawala au kuwatumikisha wananchi. Dar24 inamkariri mwalimu Suleimani Mashaka anayehoji, “katika kipindi hiki cha siku 100 ni nani amesikia kuna mtu amewekwa ndani saa 48?”

Ajira na neema kwa watumishi wa umma

Rais Samia pia amefungua mianya ya ajira na kupandisha madaraja kwa watumishi wa umma, ambao wengi wao walikuwa wameganda katika ngazi walizokuwepo kwa kipindi cha hadi miaka sita.

Juni 22, 2021, Rais Samia alitangaza kuwapandisha madaraja watumishi 70,437. Aidha, Serikali yake ilitenga Sh. 300 bilioni ili kuhakikisha kuwa kila aliyepandishwa daraja analipwa stahiki zake ipasavyo.

Aidha, kibali alichokitoa ni kwa ajili ya kupandisha madaraja watumishi 91,841. Hivyo, vicheko vitaendelea kwa watumishi wa umma wakati vibali hivyo vinaendelea kuchakatwa.

Katika sekta hiyo pia, Rais Samia amefungua zaidi milango ya ajira. Ambapo jana, Juni 26, 2021 alitangaza kutoa ajira kwa watu 9,675 katika kada ya afya na elimu. Kwa mujibu wa majina yaliyowekwa kwenye tovuti ya Ofisi ya Rais – Tamisemi ya www.tamisemi.go.tz, katika sekta ya elimu, walimu wa Sekondari na wa shule za msingi ni 6,749; na kada ya afya ni 2,726.

Neema kwa wafanyabiashara

Alipoingia madarakani, Rais Samia aliweka wazi kuwa anahitaji kupata kodi ili kuongeza kipato, lakini alisisitiza kuwa hahitaji ‘fedha zisizo halali’. Aliwataka watendaji wake na hasa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)kuhakikisha wanakaa na wafanyabiashara wanaodaiwa ili wazungumze, walipe madeni yao taratibu na waendelee na biashara zao. Alisisitiza kutotumia nguvu na kutofunga biashara. Hatua hiyo ilianza kuchukuliwa mara moja, na vicheko vikaanza kutawala kwa wafanyabiashara.

Jana, Rais Samia alikuwa mgeni rasmi katika Mkutano wa 12 wa Baraza la Taifa la Biashara, ambapo wafanyabiashara hao walimueleza kinagaubaga kuwa amefanya mabadiliko makubwa chanya na wakampongeza wakimuita ‘game changer’. Rais Samia pia alionesha kufurahishwa na jinsi walivyoridhishwa na utendaji wake.

Jana, Rais aliwaeleza kuwa Bandari ya Bagamoyo itafufuliwa na mpango wake wa ujenzi uliokuwa umesitishwa kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano sasa utahuishwa; na kazi itaendelea. Mama alisisitiza kuwa mradi wote utarudi kwenye mpango kama ulivyokuwa.

Uhuru wa vyombo vya habari na vyama vya upinzani

Tangu alipoingia madarakani, Rais Samia alionesha kuwa anahitaji vyombo vya habari viwe huru. Aprili 6, 2021, Rais Samia aliagiza vyombo vya habari hususan vya mitandaoni kufunguliwa.

“Tusiwape mdomo mdomo wa kusema tunabinya uhuru wa habari na nataka kanuni ziwe wazi, ili mtu akifungiwa ajue kosa na adhabu yake. Tusifungie tu kibabe,” alisema.

Vyombo vyote vya habari vya mitandaoni vilivyokuwa vimefungiwa vilifunguliwa. Serikali iliahidi kuwa itafanya mazungumzo na magazeti yaliyofungiwa kwa mujibu wa sheria na kuona utaratibu. Pia, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilitangaza kuwa inapanga kupunguza gharama za usajili wa leseni za vyombo vya habari vya mitandaoni kutoka Sh. 1 milioni hadi Sh. 250,000.

Kuhusu upinzani. Ni Dhahiri kuwa hata wapinzani wameonesha wazi kuwa wanaunga mkono jinsi ambavyo Rais Samia alivyosimamia uhuru wa vyama vya siasa. Hivi karibuni, kwa mara ya kwanza katika miaka mingi wakati ambao sio wa kampeni, Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe alisimamishwa na wananchi mikoa ya kusini, alipokuwa akihudhuria vikao vya ndani, na alizungumza nao kwenye eneo la hadhara.

Kusikiliza

Moja kati ya sifa za kiongozi ni kusikiliza. Rais Samia tangu alipoingia madarakani, amekutana na kuzungumza na makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na vijana jijini Mwanza, Wanawake jijini Dodoma, Wazee mkoani Dar es Salaam, Wafanyabiashara jijini Dar es Salaam na wengine wengi.

Katika mikutano hiyo yote, alitoa maamuzi mengi yaliyojibu hoja za makundi hayo. Uamuzi huo ulikuwa suluhu na kuonesha hali ya kutafuta suluhu ya changamoto nyingi zilizotajwa.

Mapambano dhidi ya corona, na afya kwa ujumla

Rais Samia aliunda Kamati maalum ya kumshauri kuhusu janga la corona. Tangu kamati hiyo ilipowasilisha mapendekezo yake, aliyafanyia kazi kwa vitendo akizingatia utaalam wa kitabibu. Amekuwa akitangaza hadharani kuwa Tanzania inakabiliwa na corona na anawataka wananchi kuchukua tahadhari. Pia, ameonesha kwa dhati kuwa anapambana kuhakikisha huduma za afya za watanzania zinaimarika.

Mashirikiano ya Kimataifa

Rais Samia ameonesha kufungua zaidi mipaka ya Tanzania, ametembelea nchi mbalimbali na kuimarisha ushirikiano. Kwa heshima, amekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania kuhutubia Bunge la Jamhuri ya Kenya. Kupitia hatua hiyo, ameshirikiana na marais wa nchi mbalimbali kuhakikisha wanaondoa vikwazo na kurahisisha maisha ya wananchi wa nchi hizo.

Rais Samia alisema kuwa bado anaendelea kuwakaribisha Mataifa ya nje kuiangalia Tanzania, na sasa amealika vyombo vya habari vya kimataifa kufanya mradi wa kuangazia uzuri wa Tanzania na kuiambia dunia walichokiona.

Hizi ni siku 100 za Rais Samia. Tunamuombea miaka minne iliyobaki iwe ya heri zaidi. Je, wewe una maoni gani?

Dodoma: Rais Samia aongea na Nandy jukwaani
Sabaya awaponza wenzake wawili, Takukuru ‘yapita nao’