Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Nishati, Januari Makamba kuhakikisha ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwaka 2023, kuhakikisha nishati safi inasambazwa kwenye taasisi kubwa nchini.

Rais Samia, ameyasema hayo hii leo Novemba Mosi, 2022 wakati akizundua mjadala wa Kitaifa wa Nishati safi ya kupikia, unaofanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Amesema, “Wakati nikiwa Makamu wa Rais, na nina bahati na January kwenye mambo ya mazingira kule nilimuelekeza taasisi zinazohudumia zaidi ya watu 300 lazima watumie nishati safi, na akiwa kule hakukaa muda mrefu akatoka hatukulitekeleza sasa nakuelekeza tena leo lilelile kwamba taasisi zile za Magereza, shule, vikosi vya ulinzi zianze sasa kujielekeza kwenye nishati safi ya kupikia.”

Rais Samia wakati akiwasili katika ukumbi wa JNICC kufungua mjadala wa Kitaifa wa Nishati safi ya kupikia.

Rais Samia ameongeza kuwa, “Sasa hivi sihesabu, maana mpo mwishoni mwishoni mkishughulikia mambo mengi ila mwaka mzima wa 2023 nataka mjielekeze kwenye hili la taasisi kubwa kutumia nishati safi ili 2024 nikirudi niwaambie Wananchi ni hatua gani nimefikia na nini nilifanya.”

Aidha, ameongeza kuwa, Ni lazima twende na Nishati Safi ya Kupikia Kwa maendeleo ya nchi, jamii yetu, haki za wanawake na wanawake Wana mambo mengi ya kujitolea kazi zao bila malipo. Tumeona akina mama wanasonga Ugali machozi yanawatoka. Nani kamlipa? Kapata fidia gani? Pengine watoto hawamtunzi. Akina mama wa aina hii wapo wengi sana na hawalipwi angalau tuwapunguzie athari wanazozipata.”

Mjadala huo wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia, unaofanyika kwa muda wa siku mbili (Jumanne Novemba 1-2, 2022), jijini Dar es Salaam umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa nishati ukilenga kujadili namna ya kumtua mama mzigo wa kuni kichwani.

Korea Kaskazini ‘yaipiga stop’ Marekani
IAEA yaanza uchunguzi wa mabomu machafu