Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemuapisha Mwalimu aliyewahi kumfundisha masomo ya Kiingereza na Hesabu akiwa kidato cha pili na cha tatu, Bi.
Khadija Mbaraka kuwa Kamishna wa Tume wa Utumishi wa Umma.

Akizungumza leo Mei 21, 2022 mara baada ya uapisho wa baadhi ya viongozi aliowateua akiwemo Bi. Khadija, Rais Samia amesema imemuwia vigumu kumuapisha Mwalimu wake huyo.

“Leo nimepata kazi kidogo kumuapisha Mwalimu wangu, Bi. Khadija, huyu bibi vyovyote alivyo mfupi, mdogo ni mwalimu wangu wa Hesabu na Kiingereza Form Two na Form Three,”amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia ameongeza kuwa ni vyema kuwashirikisha kikazi watu wa umri kama wa Bi. Khadija kwani licha ya uzee walionao lakini wapo vizuri kiutendaji na pasi na shaka wataidia kuendesha gurudumu la maendeleo.

“Wale wa umri kama kina Bi Khadija wakokoteni hivyo hivyo twende nao lakini ninajua akili iko vizuri, mimi kanifundisha akiwa kijana mdogo na nilikuwa nathubutu kusimama na kumuiga
darasani nikijua anaingia basi nakwenda kwenye blackboard na-act exactly alivyokuwa akifanya na pengine labda ndiyo maana nimekuwa hivi,” amesimulia Rais Samia.

Uapisho huu unakuja baada ya uteuzi alioufanya usiku wa kuamkia Mei 21, 2022 ambapo amemteua Balozi Ombeni Sefue kuwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), akichukua nafasi ya Halfani Ramadhani Halfan.

Pia, amemteua Halfani Ramadhani Halfani kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Prof. Rwekaza Mukandala kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), akichukua nafasi ya Bi. Gaudentia Kabaka na Yahaya Othman anayekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Mzumbe akichukua nafasi ya Prof. Mathew
Laban Luhanga ambaye alifariki Septemba 16, 2021.

Rais Samia pia amewateua watendaji wa kuu wa Taasisi Mhandisi Charles Jimmy Sangweni kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), ambaye alikuwa anakaimu nafasi hiyo na Mhandisi Modestus Martin Lumato kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Mwingine ni Eliachim Chacha Maswi kuwa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti na Ununuzi wa Umma (PPRA), akichukua nafasi ya Dkt. Irene Charles Isaka anayekwenda kutumikia wadhifa wa Mkurugenzi wa Huduma za Jamii Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mbatia afungiwa mlango Nyumbani kwake
Ugonjwa wa Monkeypox wahatarisha Ulimwengu