Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema tangu Serikali yake ilipoanza kufanya maendeleo, amethibitisha alichoambiwa na mtu mmoja mwenye busara kuwa watakaomsumbua ni wenzake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na sio wapinzani.

Akizungumza leo Ikulu wakati wa kupokea taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19, Rais Samia alieleza kushangazwa na kauli iliyotolewa na mtu aliyeaminika na kupewa mhimili, ambaye amedai sio rahisi kuamini kama angeweza kutoa kauli kama ile.

“Na hapa inanikumbusha mtu mmoja mwenye busara, nilipotwishwa huu mzigo alikuja kuniona akaniambia, ‘nimekuja kukuona, kukupa hongera lakini pia kukupa pole’. Nikamwambia napokea,” Rais Samia alianza kueleza.

“Akanipa mawaidha mengi lakini akaniambia, ‘atakayekusumbua kwenye kazi yako na kwenye uongozi wako ni shati ya kijani mwenzio na sio mpinzani. Mpinzani atakuangalia, ukimaliza hoja zao hawana neno. Lakini shati ya kijani mwenzio anayetizama mbele mwaka 2025, 2030 huyu ndiye atakayekusumbua’,” Rais Samia akakamilisha simulizi hilo.

 Akaendelea, “nataka niwambie, hiki ndicho kinachotokea, kwa sababu hauwezi kufikiria mtu mliyemuamini, mshika mhimili aende akasimame aseme yale… ni stress ya 2025.”

Rais Samia aliendelea kutoa ya moyoni kuhusu mtu huyo ambaye alieleza kuwa wamemuamini.

“Kwa sababu huwezi kuamini, mtu mzima na akili yako unaenda kubisha kuhusu tozo na mkopo wa Sh. 1.3 trilioni, kama vile ndio kwanza imetokea Tanzania wakati tangu tumepata uhuru ni mikopo kwenda mbele, na katika mikopo yote huu ni mkopo mzuri kuwahi kutokea….

“Mtu na akili yake anasimama anaongea, ni haki yake kusema chochote, lakini mtu mnayemtegemea, mtu ambaye mna matumaini naye mtashirikiana kwenye safari ya maendeleo hutegemei atasema hicho. Unategemea labda atakuwa na uelewa, kwa sababu mabajeti yote na mamikopo yote, taarifa zote za kiuchumi ndani ya nyumba yake ndio zinapita. Lakini ni homa ya 2025, wasameheni,” aliongeza.

China yawafungia ndani watu milioni 1.2 baada ya watatu kupata UVIKO-19

Kauli hiyo ya Rais imezua gumzo mitandaoni, hususan alipotaja kuwa mtu aliyeaminika na kupewa mhimili, ambapo wengi wanaamini anamzungumzia Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, ambaye hivi karibuni alizua gumzo kufuatia kipande cha video kilichosambaa kinachomuonesha akieleza kuwa kutokana na ukopaji na madeni ‘ipo siku nchi hii itapigwa mnada’.

Hata hivyo, jana, Spika Ndugai alizungumza na vyombo vya habari na kumuomba radhi Rais Samia kwa kusema haikua maana yake kumkashifu Rais. Hata hivyo, Ndugai alisema kuwa hakutoa kauli yoyote ya kukwaza bali video ilihaririwa kwa lengo la kuchonganisha.  

Tukirejea katika hotuba ya Rais Samia, aliendelea kwa kueleza kuwa wakati anakabidhiwa majukumu ya urais, wapo waliompima na kufanya tathmini zao wakaona hataweza, lakini sasa wanashangaa kuwa kile walichofikiria kimekuwa tofauti.

Alisema wakati huo, alianza kusikia kauli zinasemwa na baadhi ya wabunge kuwa hiyo ni Serikali ya mpito, hatua iliyomfanya aangalie Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujiridhisha, na hakuona jambo hilo.

“Lakini watu wakamtazama mtu aliyeshika kitabu kuapa, wakamfanyia tathmini, wakampa alama zake wakamuweka pale. Sasa yanayotokea hawaamini kwamba yule mtu waliyempa ile thamani ndiye anayeyafanya. Na kwa maana hiyo, lile tamanio lao la 2025, kwa kiwango fulani tamaa zinaondoka,” alisema Rais Samia ambaye ndiye Mwenyekiti wa CCM Taifa.

Hivi karibuni kumekuwa na mvutano usio rasmi ndani ya CCM, ambapo baadhi ya waliokuwa viongozi wameonekana hadharani wakijibizana kuhusu mwenendo wa uongozi uliopo. Baadhi ya wanachama hao wameitwa kuhojiwa kutokana na kauli zao.

Mkoa wa Kaskazini Unguja kuja na Kasi kimaendeleo
Moto wa Bunge la Afrika Kusini: Mshukiwa alikuwa na 'vilipuzi'