Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan amejitoa kimasomaso kuhakikisha kuwa Yanga inashinda nyumbani dhidi ya USM Alger ya Algeria kwa kununua tiketi 5000, ili mashabiki waingie uwanjani.

Mechi hiyo ya fainali inayosubiriwa kwa hamu imepangwa kupigwa Mei 28 katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mechi ya mkondo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema tiketi hizo ni mwendelezo wa kuongeza hamasa, ikiwa ni baada pia ya kuahidi Sh Milioni 20 kila bao la ushindi litakalofungwa na wachezaji wa Yanga kwenye mechi hizo za fainali.

“Rais Samia anahakikisha kuwa Yanga inachukua Kombe kwa kuendeleza hamasa hizi za kununua tiketi 5000 kwa lengo la kuujaza uwanja wa Taifa utakaoshuhudia mchezo mgumu wa fainali kati ya timu ya Tanzania dhidi ya USM Alger.

“Rais anawataka Watanzania waende kuujaza uwanja wa Taifa, kwa sababu mama hana mbambamba katika mbio za Yanga kuitangaza nchi kimataifa kupitia mpira wa miguu,” Amesema.

Katika hatua nyingine, Msigwa aliwataka wachezaji kuingia uwanjani kwa nguvu zote ili washinde magoli mengi kwa sababu fedha za Rais zinazotolewa ili kuibua hamasa bado zipo kwa lengo moja la kuhakikisha Yanga inaibuka kidedea katika mechi zake za fainali za Kombe la Shirikisho.

Mechi ya marudiano kati ya Yanga na USM Alger inatarajiwa kupigwa nchini Algeria, Juni 6 mwaka huu, huku timu ya Tanzania ikiingia fainali kwa mara ya kwanza katika historia ya michuano ya Kimataifa inayoendeshwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika.

Mengine makubwa yaliyofanywa na Rais Samia dhidi ya Yanga katika mechi yao ya fainali ni kuipa ndege klabu hiyo ili iende Algeria katika mechi yao ya marudiano.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Mei 23, 2023
Tembo wauwa mmoja, Wahifadhi waahidi kufanya doria