Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewasihi vijana kutokubali kutumika kwa namna yoyote katika hatua za kutafuta maendeleo ikiwa ni kisiasa au kiuchumi akikazia katika maswala ya rushwa za ngono, fedha na kutumika kuharibu amani.

Ameyasema hayo akishiriki katika kilele cha matembezi ya miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, Mkoani Kusini Pemba leo Januari 7, 2022 alipokuwa mgeni rasmi.

Rais Samia amewaambia vijana kuwa mtu anayetenda mema anajitendea mwenyewe na ndipo anapoonekana katika safu za uongozi kila inapotokea nafasi za serikali, lakini akiwakumbusha kuacha kutumika katika kila chaguzi za vyama ili waweze kupata maendeleo.

“Vijana mgeuzwa ngazi watu wanapanda tu, mnadanganywa na vifedha vidogo, na tamaa ya vinafasi, mnainamishwa migongo watu wanapanda juu ya migongo yenu, wakeshakupata wanayoyataka, hawana tena habari na nyie. Kama wote mnaowabeba, wangefanya kazi kihakililahi kuwafanyia vijana, changamoto zote tunazozungumzia vijana zingekua hazipo,” alisema Rais Samia

“Niwaombe vijana, Chaguzi zetu zote za Jumuiya na CCM zinasimamiwa na kanuni na miongozo, Vijana mna haki zote za kuchaguliwa na kuchagua, nendeni kagombeeni, Mimi nawahakikishia, zitakapokuja juu kwetu hatutatizama sura ila tutatizama uwezo, weledi na umakini wa mtu katika kufanya kazi.” Rais Samia.

Rais Samia pia amewakumbusha vijana kuendelea kusimamia miongozo ya Chama na kanuni zote ili chaguzi za CCM mwaka huu ziwe za haki.

“Vijana katika chaguzi zenu, kunatawala fitna, rushwa, na mambo kadhaa, ukifika chaguzi za vijana sisi wenye watoto wa kike roho zetu titititii…Na risala yenu mmesema mnaenda kupinga udhalilishaji na unyanyasaji, mwanamke na mwanaume wote wakisimama wana uwezo sawa. Acheni kunyanyasa ndugu zenu, acheni kudhalilisha dada zenu, anaesimama ana sifa apewe nafasi ya uongozi. Kwa hiyo niwaombe vijana yale mliyoyazoea acheni, nendeni kasimameni fanyeni kazi yenu.” aliongeza Rais Samia.

Katika kukazia nguvu kazi ya vijana Rais Samia aliendelea kuwaomba vijana kutoachia nafasi ya kutumika kupasua Chama akisisitiza kuwa kwa sasa UVCCM wanaweza kuyafanya mambo yote kwa uhuru kwa kuwa CCM ipo imara, na itakapotokea chama kimepasuliwa vijana hawatapata nafasi ya kufanya yote wanayofanya leo.

Rais Samia amekazia ukweli wa kuwa vijana ndio nguvukazi kubwa ya taifa yenye umuhimu kwa taifa lolote, wabeba maono, wenye ubunifu, walitoa mchango mkubwa katika kukomboa taifa.

“Hivyo basi uhai, usalama, na maendeleo na ustawi wa taifa lolote unatagemea vijana. Sasa hivyo ni kwa upande vijana hawa wamelelewa vizuri, wamefunzwa itikadi na sera na mambo yote ya nchi yao. Lakini vijana wakiyakosa hayo fikirieni vjiana hao watakuwaje na nchi itakuaje? Aliwauliza uma uliokua unamsikiliza.

Rais Samia pia amewataka vijana wote ambao hawana ajira wawe wavumilivu kwa kusubiri ajira tofauti ambazo serikali inatoa kupitia miradi ya serikali katika sekta tofauti zinazoleta maendeleo ya nchi wakati akiwaahidi kuwa serikali itafungua vyuo vya amali ili vijana kujiajiri kwa kutafuta fursa za kazi zinazojitokeza katika sekta mbalimbali na kuanza kuzitumia kabla ya kusubiri ajira rasmi.

Aidha Rais Samia amewataka vijana waendelee kupata chanjo ya UVIKO 19 ili waendelee kufanya shughuli za kujiingizia kipato na za kuleta maendeleo.

“Ukichanja, narudia ninalosema kila siku, sio kila ukichanja hutapata ugonjwa huo tena, bali mwili wako utakua na ustahmilivu ambapo ni tofauti na ambae hajachanja, wapo waliopata ugonjwa wakiwa wamechanja na hawakusumbuka. Langu ni kuwahimiza chukueni tahadhari, Maradhi haya sio ya mchezo, yana makali yake lakini ukichanja yanapunguza makali.” alisema.

Vijana wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi UVCCM, wamekua na kawaida ya kufanya matembezi, usafi na kuzindua miradi tofauti ya vijana wiki moja kabla ya sherehe za kiserikali ikiwa wakati huu ni visiwani Zanzibar katika kusherehekea Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yanayofanyika kila Januari 12 wakiwa na kauli mbiu inayosema “Uchumi wa buluu ni fursa yetu vijana tutumie ipasavyo”.

Fraga awekewa ngumu kujiunga Simba SC
Simba SC yatoa onyo kali Jezi Feki