Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, David Silinde amesema katika kipindi cha miaka miwili tangu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, serikali imenunua madume ya ng’ombe ya kisasa 366 yenye thamani ya Silingi Milioni 878.4 ili kuboresha mifugo nchini.

Silinde ameyabainisha hayo (20.03.2023) katika Kata ya Dakawa iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro, wakati wa hafla fupi ya kugawa madume 40 kwa vikundi vya wafugaji 20 ili kuboresha mifugo yao ya asili katika wilaya hiyo.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, David Silinde akipeana mkono na mmoja wa wawakilishi wa vikundi vya wafugaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro, waliopatiwa madume bora ya ng’ombe wa kisasa ambapo katika vikundi 20 kila kikundi kimepatiwa madume mawili kwa ajili kupandia ng’ombe jike ili kuboresha mifugo yao ya asili.

Amesema, “Rais Dkt. Samia amekuwa akifanya kazi nzuri katika kipindi kifupi kwenye Sekta ya Mifugo akiwa na lengo la kuinua wafugaji nchini kwa kuwa na mifugo bora na kisasa, Rais anapowanyanyua wafugaji anataka wananchi kuwa na maisha bora na amekuwa akihangaika katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja.”

Silinde ameongeza kuwa, uwepo wa madume bora ya kisasa ya ng’ombe ambao wamesambazwa maeneo mbalimbali nchini, ng’ombe watakaotokana na madume hao watakuwa na nyama nyingi na kufungua fursa zaidi za upatikanaji wa nyama kwa wingi kwa ajili ya kuuza ndani na nje ya nchi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, David Silinde akikagua madume bora ya ng’ombe 40 kati ya 366 ambao serikali imenunua kwa Shilingi Milioni 878.4 na kusambaza katika vikundi vya wafugaji katika halmashauri nane kwenye mikoa minane ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro ambayo ina wafugaji wengi, ikiwa na lengo la kuboresha mifugo ya asili kwa ng’ombe watakaozaliwa kupitia madume hao.

Akimwakilisha Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Afisa Mifugo Mkuu, Basil Mataba amesema ng’ombe hao 366 wamegaiwa kwenye halmashauri nane katika mikoa minane ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ambayo ina wafugaji wengi.

Amesema, licha ya ugawaji wa madume hayo kwa vikundi vya wafugaji lakini mafunzo yamekuwa yakitolewa namna ya kuwatunza na kufuatilia matumizi yake pamoja na kutatua changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kujitokeza.

Afisa Mifugo Mkuu Bw. Basil Mataba katika hafla fupi ya kugawa madume 40 kwa vikundi vya wafugaji 20 katika Kata ya Dakawa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro, amevitaka vikundi hivyo kutouza madume hayo wala kuyatumia katika matumizi mengine yakiwemo ya kilimo badala yake yatumike kwa ajili ya kupandia ng’ombe jike ili kuboresha mifugo yao ya asili.

Aidha, ametoa maelekezo ya namna vikundi vinapaswa kutunza madume hayo kwa kutotumiwa katika shughuli nyingine ikiwemo ya kilimo kwa kuwa serikali imenunua na kusambaza madume kwa vikundi vya wafugaji kwa ajili ya kupandishia ng’ombe jike pekee na vikundi haviruhusiwi kuuza madume hayo.

Baadhi ya wawakilishi wa vikundi vya wafugaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro, wameipongeza Serikali kwa kuwapatia madume ya n’gombe bora wa kisasa ambao wataenda kubadilisha ubora wa ng’ombe wao watakaoazaliwa kupitia madume hayo.

Young Africans: Tunamtaka yoyote Kombe la Shirikisho
Samatta na wenzake watua kambini Misri