Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaagiza watendaji wa serikali kujituma kufanya kazi akisisitiza kuwa atawachukulia hatua wale wasiowajibuka ipasavyo.

Rais Samia ameyasema hayo leo Jumanne Aprili 6, 2021 wakati akiwaapisha Makatibu Wakuu, Manaibu Makatibu Wakuu wa Wizara na Wakuu wa taasisi na Idara mbalimbali za serikali, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

“Nendeni mfakanye kazi….Mimi ni Mama Wewe ni Kijana Ukinizingua Tutazinguana,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia ameagiza wananchi wasizuiwe kuelezea kero zao na kwamba endapo viongozi wa kitaifa watakutana na mabango katika ziara zao atawaondoa kazini Mkurugenzi wa Halmashauri husika na Mkuu wa Wilaya.

“Kwa sababu najua tunapokuja watu wanakuja na mabango mbio mnakwenda kuyakusanya na kuwanyuka watu kuwapelekea mnapokujua nyie ili wasiseme yao yanayowasibu , naomba kero za wananchi zikashughulikiwe, tunapokuja na kukuta bango moja mkuu wa wilaya au mkurugenzi umekwenda na tukikuta malalamiko kwamba mnawafinya wananchi wasiseme hivyo hivyo tutashughulikiana,” amesema Rais Samia.

Amesema imekuwa ni kawaida viongozi wakifanya ziara mikoani na wilayani wanapokewa na mabango ya wananchi wakilalamikia kero mbalimbali na masuala wanayolalamikia si ya kitaifa, huku wananchi wanaothubutu kuonesha kero zao kupitia mabango wanakamatwa, wakati mabango yale mengine wala siyo masuala ya kushughulikiwa katika ngazi za juu bali ya kushughulikwa katika ngazi za chini.

“Kwa hiyo naomba tunapokuja huko mimi na Makamu wa Rais, Waziri Mkuu tukikuta mabango basi yawe mambo ya kitaifa lakini siyo mambo ya kushughulikiwa kule chini, nataka niseme bango moja aidha Mkurugenzi au Mkuu wa Wilaya amekwenda na hii haina maana mkazuie watu kuandika kero zao,” amesisitiza Rais Samia.

Niyonzima: Simba SC mjiandae kisaikolojia
CAF yaja na mpango mpya vipimo Covid-19