Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka wanawake wote nchini Tanzania kuweka mipango mizuri katika uchaguzi wa mwaka 2025 ili waweze kumuweka mwanamke Rais madarakani kwani nafasi aliyonayo sasa ni kutokana na nguvu za mwenyezi Mungu.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Septemba 15, 2021 wakati akihutubia katika maadhimisho ya siku ya Demokrasia duniani yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam.

“Sasa ndugu zangu rais mwanamke tutamuweka 2025, tukifanya vitu vyetu vizuri tukishikamana tukimweka rais wetu tutakutana hapa kwa furaha kubwa sana, wameaanza kutuchokoza, kuandika kwenye vigazeti Samia hatasimama nani kawaambia,” Amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema kuwa licha ya kupewa tuzo na majukwaa mbalimbali ya wanawake waliohudhuria maadhimisho hayo bado wanawake hawajamuweka Rais madarakani.

“Fadhila za Mungu zikija mikononi kwako usiziachie, hizi ni fadhila za Mungu ndugu zangu wanawake wamefanya kazi kubwa kuleta uhuru wa nchi hizi, wanawake tumefanaya kazi kubwa kujenga siasa za nchi hizi, tumebeba sana wanaume  katika siasa za nchi hizi leo Mungu ametupa baraka mikononi tukiiachia Mungu atatulaani.” Amesema Rais Samia.

Rais Samia aliapishwa kuwa rais Machi 19, 2021 baada ya kifo cha aliyekuwa rais wa awamu ya tano, John Magufuli. Kabla ya kupokea kijiti hicho,  Samia alikuwa makamu wa Rais wa Tanzania. Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania,  rais akifia madarakani,  makamu wa Rais huapishwa kuwa Rais.

Atakayevunja sheria atashughulikiwa - Rais Samia
Kamwaga: Simba watajaza uwanja jumapili