Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dtk. Ali Mohamed Shein amefurahishwa na mapinduzi yanayofanywa na wanawake katika sekta ya elimu.

Akizungumza leo katika shule ya msingi Kihinani mkoa wa Mjini Magharibi, alipokuwa akiweka jiwe la msingi la jengo la shule hiyo , Rais Shein amesema kuwa amefurahi kusikia kuwa idadi ya wanafunzi wa kike katika shule hiyo ni kubwa kuliko idadi ya wanafunzi wa kiume, na kwamba kati ya walimu wote wa shule hiyo ni mwalimu mmoja pekee ndiye mwanaume.

Alisema kuwa kinachofanyika hivi sasa ni mapinduzi ya elimu kwani hivi karibuni alishiriki mahafali ya chuo kimoja visiwani Zanzibar na kushuhudia nafasi nne za juu zikishikiliwa na wanawake pekee.

Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohamed Mahmoud, shule ya msingi Kihinani

“Haya ni mapinduzi katika elimu. Leo wanawake wanawashinda wanaume kwenye masomo tena sio yale marahisi. Zamani wanawake walikuwa wanachukuliwa kama wako nyuma kwenye elimu na hata wakisoma masomo yao ni yale ya kiingereza na Kiswahili, lakini hivi sasa ni tofauti,” alisema Rais Shein na kuwaasa wanawake kuendelea kuweza hata bila kusubiri kuwezeshwa.

Aidha, Rais Shein aliwaasa wanafunzi wa shule ya msingi kuzingatia masomo na kuachana na mambo yasiyofaa au kutamani mambo ambayo yako kinyume na umri wao.

“Fuatilieni masomo muachane na mambo yasiyofaa. Elimu ni nyenzo kubwa sana, iwe elimu dunia na elimu akhera. Na ndio maana nikaruhusu elimu bure. Sisi tuliambiwa na wazazi wetu tusome kwa bidii na tukafanya hivyo,” alisema Dkt. Shein.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amani, Khadija Bakari alimueleza Rais Shein kuwa jengo la shule hiyo lililogharimu kiasi cha shilingi milioni 64,  limejengwa kwa ushirikiano kati ya wananchi na Serikali.

Alifafanua kuwa wananchi walichangia kiasi cha shilingi milioni 24 na Serikali shilingi milioni 40.

Dkt. Shein aliwapongeza wananchi kwa ushirikiano wao na kuwataka kuendelea na moyo huo kwa kuwezesha miundombinu kwani Serikali imetoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari ili kuinua sekta ya elimu.

Picha: Simba waanza mkutano wa mabadiliko
picha mbalimbali za Simba katika mkutano wa mabadiliko ya kifikra za soka nchini