Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kulikatia fedha shirika la afya Duniani WHO ambapo amesema shirika hilo halikutilia maanani kwa namna ilivyopasa hatari ya maambukizi ya virusi vya corona, amelilaumu shirika hilo kwa kuegemea zaidi upande wa China.

Trump amedai kwamba asasi hiyo ya kimataifa ilishirikiana na China katika miezi kadhaa iliyopita kupunguza hatari ya maambukizi ya virusi vya corona.

Katika bajeti ya mwezi Februari utawala wa Trump ulipendekeza kupunguza mchango wa fedha wa Marekani kwa shirika la WHO kutoka dola milioni 122.6 hadi dola milioni 59.9

Aidha amesema Shirika hilo limeisifu China ingawa pana sababu ya kuwa na mashaka juu ya idadi rasmi  iliyotolewa na serikali ya China juu ya vifo vilivyotokana na mambukizi ya virusi vya corona.

Ikumbukwe kuwa Shirika hilo la kimataifa lililitangaza mlipuko wa maambukizi ya virusi vya corona kuwa hatari kwa afya ya binadamu wote, tarehe 30 mwezi Januari, takribani mwezi  mmoja kabla ya rais wa Marekani kusema kwenye “twitter” kwamba maambukizi ya virusi vya corona yalikuwa yamedhibitiwa nchini Marekani.

Mpaka sasa watu zaidi ya alfu 12 wameshakufa kutokana na maambukizi  ya virusi vya  corona nchini Marekani na wataalamu wa masuala ya afya wamesema idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka wiki hii nchini Marekani.

Benki yashikilia nyumba za Jeff Koinange kupigwa mnada
Mgonjwa mpya wa Corona Kenya alitembelea Tanzania