Moja kati ya matukio yaliyopata nafasi kubwa kwenye vichwa vya habari duniani wiki hii ni pamoja na uamuzi wa Rais wa Equatorial Guinea, Teodoro Obiang Nguema kumteua mtoto wake, Teodorin Nguema Obiang kuwa makamu wake.

Kituo cha runinga cha Taifa hilo kilitoa tangazo la uteuzi huo Jumatano wiki hii, tangazo ambalo lilipokelewa kwa hisia tofauti na wananchi wa Taifa hilo.

“Kwa mujibu wa katiba ya Equatorial Guinea, ninamteua mheshimiwa Teodorin Nguema Obiang kuwa Makamu wa Rais atayehusika na ulinzi na usalama,” tamko la Rais lilisomwa na kituo hicho cha runinga.

Mtoto huyo wa Rais ana umri wa miaka 47 na kabla ya kupandishwa katika nafasi hiyo, alikuwa Makamu wa pili wa rais tangu mwaka 2012 na hivi sasa anaonekana ndiye anayeandaliwa kumrithi rais huyo.

Rais Teodoro Obiang Nguema amekuwa madarakani tangu mwaka 1976 na alichaguliwa tena Aprili mwaka huu kwa kupata asilimia 93.7 ya kura zote halali. Anatarajiwa kutangaza sehemu iliyobaki ya baraza lake la Mawaziri ndani ya wiki mbili.

Video: RC Paul Makonda amezisimamisha Kampuni nne
Video: Tukio zima la Mbunge Goodluck kuvuliwa ‘baraghashia’ live - CCTV camera