Rais wa klabu ya Inter Milan, Erick Thohir, yupo katika mazungumzo mazito na meneja wa klabu hiyo Roberto Mancini, yaliyolenga kumtaka asalie klabuni hapo na kuachana na ofa ya kutaka kukabidhiwa kikosi cha timu ya taifa ya Italia.

Mancini, amekua akihusishwa na taarifa za kuwa miongoni mwa makocha wanaofikiriwa kukabidhiwa kikosi cha The Azzurri, ambacho kitakua hakina mkuu wa benchi la ufundi mara baada ya kumalizika kwa fainali za barani Ulaya (Euro 2016), kufuatia Antonio Conte kupata kibarua katika klabu ya Chelsea.

Rais wa Inter Milan, Thohir ameonyesha kuridhishwa na kazi zinazofanywa na Mancini tangu alipompa ajira mwaka 2014, ambapo kwa msimu huu amefanikiwa kurejesha heshima ya klabu hiyo kuwa miongoni mwa vilabu vitakavyocheza michuano ya barani Ulaya msimu wa 2016-17.

Thohir, anaamini endapo atakubali kumuachia meneja huyo ambaye aliwahi kupita Man City na kutwaa ubingwa wa England, atakua amefanya kosa kubwa kutokana na kuhofia Inter Milan kurudi nyuma kisoka.

Hata hivyo mpaka sasa haijafahamika mazungumzo ya wawili hao yamefikia katika hatua gani, lakini tajiri wa Inter Milan ameonyesha kutokua tayari kumuona Mancini akikubali kuondoka na atakuwa tayari kumugharamia kwa lolote atakalolihitaji.

Roy Hogdson Atangaza Kikosi Cha England, Amtema Walcott
AS Monaco Waahidi Kumsuka Upya Radamel Falcao