Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa siku 7 kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kulipa deni la bilioni 2 ambalo wanadaiwa na Shirika la nyumba la Taifa (NHC).

Dkt. Magufuli ametoa agizo hilo kwa Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Injinia Joseph Nyamhanga leo jijini Dar es Salaam katika ziara ya kushtukiza ya kuangalia ujenzi wa hosteli za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Nawapa siku 7 muwe mmelilipa hilo deni huku mkiendelea na utaratibu wa kuhamia Dodoma, kama hamtalilipa kwa wakati nitawaagiza NHC kuwatolea vitu vyenu nje kama wanavyofanya kwa wengine,” alisema Dkt. Magufuli.

Amesema kuwa kiwango hicho cha bilioni 2 kingeiwezesha wizara hiyo kujenga ofisi za wizara kwa kuwatumia Wakala wa Majengo (TBA) ambao wako chini ya wizara hiyo badala ya kutumika kama kodi ya pango.

Aidha, ameitaka wizara hiyo kuhamia Mjini Dodoma mara tu watakapokamilisha deni hilo na kutoendelea kupanga jijini Dar es Salaam, kwani hakuna sababu ya kuendelea kupanga majengo ya ofisi Dar es Salaam wakati Serikali yote inahamia Dodoma.

Wakati huohuo, Rais Dkt. Magufuli ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Tecknolojia, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na  Wakala wa Majengo (TBA) na uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kusimamia  vizuri mradi wa ujenzi wa hosteli za chuo kikuu ambao Rais mwenyewe aliahidi shilingi bilioni 10 katika ujenzi huo, bilioni 5 imekwishatolewa na bilioni nyingine 5 itatolewa ndani ya wiki hii.

Hosteli hizo zinategemea kuchukua wanafunzi 4000 ambapo itapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la wanafunzi kukaa nje ya maeneo ya chuo.

Prof. Muhongo Asema Sekta ya Madini Inachangia Asilimia 3.5 ya Pato La Taifa
Mhadhiri Wa Chuo Kikuu Dkt. Bashiru Ally Aema Hakuna Udikteta Serikali ya Awamu ya Tano