Rais wa Malawi, Peter Mutharika wikendi iliyopita alimshukia muhubiri maarufu nchini Nigeria, T.B Joshua wa kanisa la Synagogue Church of All Nations (SCOAN) kufuatia taarifa kuwa mhubiri huyo amemtabiria siku ya kifo chake.

Taarifa ambazo hazijathibitishwa zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii, zinadai kuwa T.B Joshua ametabiri kuwa Rais huyo wa Malawi pamoja na Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe watafariki kabla ya April 1 mwaka huu.

Akiongea kupitia Kituo cha Runinga cha Taifa hilo, Rais Mutharika alisema kuwa mhubiri huyo ni muongo na kwamba wakati huu utabiri wake utashindwa, tofauti na utabiri alioutoa mwaka 2012 wa kifo cha kaka yake uliofanikiwa.

“Ngoja nikueleze Joshua… utashindwa. Ulichokifanya mwaka 2012 hakitatokea tena mwaka huu,” alisema Mutharika.

Mwaka 2012, T.B Joshua alitabiri kuwa kifo cha rais mmoja wa Kusini mwa Afrika ambaye hakumtaja jina, lakini kaka yake rais wa sasa, ambaye alikuwa rais wa Malawi wakati huo, Bingu Mutharika alifariki ndani ya kipindi kilichotabiriwa.

Rais huyo wa Malawi alienda mbali na kueleza kuwa kama kweli T.B Joshua ni nabii anayeona matukio ya mbele, kwanini alishindwa kuona tukio la kuanguka kwa jengo la kanisa lake jijini Lagos mwaka 2014 lililochukua uhai wa watu 116.

“Kwanini hakuona tukio hilo baya? Hii inaonesha kuwa ni muongo. Anataka tu kujipatia fedha,” alisema Rais Mutharika.

Video: Wamarekani watumia Wimbo wa Kendrick Lamar Kumpinga Donald Trump
Takukuru waanza kuchunguza sakata la Rushwa kwa Lukuvi