Rais wa Misri Abdul Fattah al-Sisi amewazawadia wachezaji wa timu ya taifa ya nchi hiyo dola za kimarekeani 85,000 kila mmoja, baada ya kufanikisha lengo la kuivusha nchi hiyo kwenye mtihani wa kucheza fainali za kombe la dunia za 2018, ikitokea ukanda wa Afrika.

Kikosi cha Misri kilichomoza na ushindi wa mabao mawili kwa moja usiku wa kuamkia leo dhidi ya timu ya taifa ya Congo Brazzaville, na kumaliza kasumba ya kutoshiriki fainali hizo kubwa tangu mwaka 1990.

Rais Fattah ametangaza zawadi hiyo kwa wachezaji leo jumatatu baada ya kukutana na kikosi cha Mafarao sambamba na kocha wao kutoka nchini Agentina Hector Cuper.

“Labda hatukucheza soka la kuvutia, lakini kubwa tumefanikiwa kufuzu katika fainali za kombe la dunia, na jambo hilo limekua faraja kubwa kwa kila raia wa nchi hii,” alisema kocha Cuper.

Rais Fattah pia amechukua muda wake binafsi kumpongeza shujaa wa mchezo wa jana mshambuliaji wa klabu ya Liverpool Mohamed Salah, ambaye alifunga bao la ushindi kwa njia ya mkwaju wa penati katika dakika za lala salama, na kuiwezesha Misri kutinga fainali za kombe la dunia zitakazounguruma nchini Urusi.

“Ninajivunia wachezaji wa timu hii ya taifa, lakini shukurani za kipekee ziende kwa Mo Salah, ambaye ametufanya tuonekane katika ulimwengu mzima na kutambuliwa kama washiriki wa fainali za kombe la dunia za 2018, kwa mpira wa penati alioupiga dakika za mwisho,” alisema rais Fattah.

“Pia ninamshukuru sana kocha Cuper ambaye amezifanya ndoto zetu kuwa kweli.”

Mbali na mafanikio ya kucheza fainali za kombe la dunia baada ya miaka 28, timu ya taifa ya Misri (The Pharaohs), inajivunia rekodi ya kutwaa ubingwa wa kombe la Afrika mara saba.

Hii inakua mara ya tatu kwa misri kushiriki fainali za kombe la dunia, baada ya kufanya hivyo kwa mara ya kwanza mwaka 1934 na kisha 1990.

Waasi washambulia kambi ya UN nchini DR Congo
France Football waendelea kutaja watakaowania tuzo ya Ballon d'Or