Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir amewaonya watu wanaopanga mitandaoni kufanya maandamano ya kuiangusha serikali yake akidai kuwa watakutana na pingamizi lenye nguvu.

Kwa kipindi cha wiki mbili sasa, kundi jipya linalojiita ‘Vuguvugu la Red Card’ (Red Card Movement) limekuwa likisambaza jumbe kwenye mitandao ya kijamii kwa lengo la kuhamasisha maandamano ya kupinga serikali ya Kiir wakitumia hashtags #KiirMustGo na SouthSudanUprising.

Viongozi wa uhamasishaji wa maandamano hayo wanaonekana kuwa ni raia wa nchi hiyo waishio nchi za nje.

Vuguvugu hilo linaonekana kuanzishwa kutokana na jinsi ambavyo vuguguvu la kumuondoa madarakani Omar Al-Bashir nchini Sudan lililoanzia mitandaoni lilivyofanikiwa.

Rais Kiir ameeleza kuwa mabadiliko yoyote nchini humo yatafanyika kwa kuzingatia njia za kidemokrasia na sio vinginevyo na kwamba njia nyingine yoyote itakayoanzishwa itajibiwa kwa pingamizi kali la nguvu.

“Njia ya kufikia hali ya utulivu Sudan Kusini ni kupitia demokrasia na uchaguzi wa kidemokrasia pekee, na hiki ndicho tunachopigania na hatutakiharibu,” alisema Rais Kiir.

Waandishi wa habari wa Reuters wameeleza kuwa tangu wiki iliyopita, kumekuwa na ongezeko kubwa la maafisi wa polisi walioimarisha ulinzi kwenye mitaa ya jiji la Juba.

Hata hivyo, maafisa wa polisi walieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kuimarisha ulinzi katika kuelekea maadhimisho ya uhuru wa Sudan Kusini uliopatikana mwaka 2011.

Msemaji wa jeshi la ulinzi, Jenerali Lul Ruai Koang ameiambia AFP sherehe za awali za maadhimisho hayo zimesitishwa kwa ajili ya hatua ya mwisho ya maandalizi ya tukio husika.

“Lengo la kuweka ulinzi mkali ni kuhakikisha kuna usalama kwa watu wetu wakati wote wa sherehe za maadhimisho ya siku ya uhuru,” alisema Jenerali Koang.

Kituo binafsi cha radio cha Eye Radio kiliripoti jana kuwa katika baadhi ya maeneo ya jiji la Juba, wakaazi wamekuwa wakiamshwa usiku wa manani na vyombo vya usalama vilivyopita nyumba kwa nyumba kusaka silaha za moto.

China: Ghorofa laanguka na kuua
Watu 80 wakamatwa kwa kula mchana wakati wa Ramadhan

Comments

comments