Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amemsihi Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amuepuke Mtu yoyote anayejiita Chawa wake kwakuwa Machawa wengi wamejaa unafiki na uongo na hawana nia njema ya kumsaidia Rais Samia kuwa Kiongozi bora na kuisaidia Serikali kutimiza wajibu wake.

Akiongea Mjini Moshi leo wakati wa Kongamano la BAWACHA ambalo Mgeni rasmi wake ni Rais Samia, Mbowe amesema “Mh. Rais nilipotangaza ujio wako kwenye Kongamano la BAWACHA, wengi waliamini pengine ni utani, wengi walipokea kwa hisia tofauti chanya na hasi, yote hiyo ni uthibitisho wa namna Taifa letu linavyoishi kwa hofu, kwa utengano, kwa kutopendana na kutoaminiana.”

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA, Freeman Mbowe.

“Mh. Rais unafiki na uongo ulaanisha Taifa, Taifa letu lina Watu wengi wasiosema na kuuishi ukweli, hili ni chimbuko kubwa la mporomoko wa maadili, nakusihi sana Mama epuka Mtu yoyote anayejiita Chawa wako.”

“Mh. Rais sisi wengine tumechagua kusema ukweli na kukataa dhambi ya unafiki, tumelipa gharama kubwa kwa misingi na misimamo yetu hiyo, tunaamini ukweli, uwazi, kutokuwa Wanafiki ndio njia bora ya kukusaidia uweze kuwa Kiongozi bora na kuisaidia Serikali yako iweze kutekeleza wakibu yako.”

Mke arejea nyumbani baada ya miaka miwili, Mumewe achekelea
Mimi ni Rais wa Watanzania wote: Rais Samia