Rais wa Klabu Bingwa Tanzania Bara ‘Young Africans’ Injinia Hersi Said, ametoboa siri ya kuwasainisha mikataba mipya baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo katika kipindi hiki cha kujiandaa na Msimu Mpya.

Wachezaji Yanick Bangala na Djuma Shaban wamesaini mkataba mpya na klabu hiyo hadi mwaka 2024, huku Mshambuliaji Fiston Mayele akiwa katika hatua za mwisho kukamilisha mpango huo.

Hersi amesema Young Africans imejizatiti kuendelea kuwa na kikosi Bora na Imara, hivyo haitakubali kuwaachia Wachezaji wao nyota ambao msimu uliopita walidhihirisha kuwa na kiwango cha kuisaidia timu yao.

Amesema mbali na Wachezaji hao, Uongozi wake unaendelea na mchakato wa kusaini Mikataba mipya na Wachezaji wengine ambao mikataba yao ya sasa inaelekea ukingoni (ima kwa kubaki Mwaka mmoja au Miezi Sita).

“Hatutaruhusu mchezaji yeyote muhimu kuondoka Young Africans. Kwa wale wote mikataba yao inatarajiwa kumalizika na iliyomalizika tutawaongezea.”

“Hivyo tumemuongezea mkataba Bangala ambao rasmi utakuwa unamalizika mwaka 2024. Tunafurahia kuona akiendelea kubakia hapa,” amesema Hersi.

Yanick Bangala

Inaeleezwa kuwa Mchezaji Kiraka Yannick Bangala, amesaini Mkataba mpya na klabu hiyo wenye Thamani ya Shilingi Milioni 400.

Bangala aliyefanikiwa kutwaa Tuzo ya Kiungo Bora wa Ligi Kuu Bara 2021/22, ameongeza mkataba wa mwaka mmoja ambao utaendelea kumuweka Young Africans hadi 2024 baada ya ule wa awali kutarajiwa kuisha 2023.

Nyota huyo mwenye uwezo wa kucheza beki wa kati na kiungo mkabaji, alijiunga na Young Africans mwanzoni mwa msimu wa 2021/22 akitokea FAR Rabat ya Morocco.

Odinga aongoza kura za maoni
Kocha Nabi aitolea uvivu Bodi ya Ligi, TFF