Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma jana alinusurika kung’olewa katika kiti cha urais wa nchi hiyo kupitia kura za kutokuwa na imani naye zilizopigwa na wabunge wa nchi hiyo.

Kampeni ya kumng’oa Zuma madarakani kupitia kura ilianzishwa na wabunge wa upinzani baada ya Mahakama ya Juu nchini humo kueleza kuwa alikiuka Katiba ya nchi kwa kutofuata maamuzi ya mahakama yaliyomtaka  kurudisha fedha za umma alizozitumia kukarabati jumba lake la kifahari.

Wabunge wa chama tawala cha African National Congress (ANC) ambao ni zaidi ya theluthi mbili ya idadi ya wabunge wote ndio waliomuokoa kwa kumpigia kura nyingi za kumtaka abaki madarakani. Zuma alipata kura 233 zinazomuunga mkono dhidi ya kura 143 zilizotaka aondoke.

Hata hivyo, pamoja na ushindi huo bungeni, bado Zuma anakabiliwa na msukumo mkali kutoka kwa wanaharakati na vyama vya upinzani nchini humo kumtaka aondoke mwenyewe kutokana na kuharibika kwa heshima yake kufuatia kashfa hiyo nzito.

Mbali na kashfa hiyo, Rais Zuma pia anakumbwa na kashfa ya kushirikiana na familia tajiri ya Gupta ambayo inadaiwa kuwa na ushawishi juu ya uchaguzi wa mawaziri na viongozi wengine wa ngazi za juu wa serikali yake.

 

 

Rais Mpya wa FIFA akumbwa na Kashfa ya Rushwa, ashinikizwa kujitumbua Jipu
Serikali yaweka wazi Mshahara wa Kikwete alipokuwa Rais