Mwamuzi Ramadhan Kayoko ndiye atachezesha mechi ya Ngao ya Jamii baina ya Simba na Yanga itakayochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Jumamosi hii.

Habari kutoka ndani ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zimefichua kuwa Kayoko ndiye atashika kipyenga katika mechi hiyo ya ufunguzi wa msimu.

“Kamati ya waamuzi imeshafanya uteuzi wake na refa wa mechi hiyo atakuwa ni Ramadhan Kayoko kutoka Dar es Salaam,” kilifichua chanzo chetu

Kwa mujibu wa chanzo hicho, Kayoko atasaidiwa na refa msaidizi namba moja Frank Komba, refa msaidizi namba mbili Soud Lila na refa wa akiba Heri Sasii wote wakitokea Dar es Salaam.

Hiyo ni mechi ya kwanza ya Watani wa Jadi kuchezeshwa na Kayoko tangu alipopata Beji ya Uamuzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) mapema mwaka huu

Refa huyo ndiye aliyechezesha mchezo wa kimataifa wa kirafiki wa kuadhimisha tukio la Wiki ya Mwananchi uliofanyika Agosti 29 ambao Yanga ilipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Zanaco ya Zambia.

Lakini pia Kayoko ndiye aliyechezesha mechi ya kuadhimisha kilele cha Tamasha la Simba Day, Septemba 19 ambao Simba ilichapwa bao 1-0 na TP Mazembe ya DR Congo.

Mwaka jana Kayoko alichezesha mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam baina ya timu hizo mbili ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-1.

Biden, Macron kukutana uso kwa macho mwishoni mwa Oktoba
PSG kumkosa Messi