Kiungo kutoka nchini Brazil, Ramires Santos do Nascimento, amevunja ukimya kwa kusema kilichomuondoa Chelsea na kujiunga na klabu ya Jiangsu Suning, inashiriki ligi kuu ya soka nchini China.

Ramires aliondoka Chelsea wakati wa dirisha dogo la usajili, mwezi januari mwaka 2016 kwa ada ya uhamisho wa Pauni million 25, baada ya kuitumikia klabu hiyo ya magharibi mwa jijini London kwa kipindi cha miaka sita.

Kiungo huyo aliyekua sehemu ya mafanikio ya kuiwezesha The Blues, kutwaa ubingwa wa barani Ulaya mwaka 2012, amesema kikwazo kikubwa kilichomfanya aondoke Stamford Bridge, ni ujio wa meneja wa muda Guus Hiddink ambaye alichukua mikoba ya Jose Mourinho aliyetimuliwa mwishoni mwa mwaka 2015.

Amesema tangu alipowasili meneja huyo kutoka nchini Uholanzi, maisha ya soka lake ndani ya Chelsea yalibadilika kutokana na Hiddink kutomuweka kwenye mipango yake ya mara kwa mara, hali ambayo ilimnyima nafasi ya kujumuika na wengine kwenye kikosi cha kwanza.

Amesema hali hiyo ilimuuwia vigumu kuvumilia, kutokana na kufahamu wazi kwamba alikua na uwezo mkubwa wa kusaidina na wengine kupambana uwanjani, kama ilivyokua utawala wa Jose Mourinho kabla hajaondoka.

Hata hivyo Ramires amedai kwamba pamoja na madhila hayo, alijikaza kisabuni na kuamini ipo siku angeodoka klabuni hapo, kufuatia kufahamu fika hakuwepo kwenye mipango ya meneja huyo.

“Nilivumilia mambo mengi yaliyonisibu nikiwa Chelsea, na wakati mwingine nilitamani kuondoka nje ya muda wa dirisha la usajili lakini hali hiyo ilishindikana kufuatia taratibu za uhamisho kunibana.” Alisema Ramires

Lakini pamoja na kuanika wazi mapungufu ya meneja wa muda wa klabu hiyo inayomilikiwa na tajiri wa kirusi Roman Abramovic, Ramires amesema bado ni shabiki mkubwa wa Chelsea na kila inapocheza huifuatilia.

“Hata hii leo, mimi bado ni shabiki mkubwa wa Chelsea, na ninatamani sana klabu hii irejee katika makali yake kutokana na hali ngumu inayopitia kwa sasa ambayo inainyima nafasi ya kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.

“Sina budi kumshukuru kila mmoja alienipa ushirikiano wakati nipo Chelsea, na ninaamini jambo hilo ndilo limenifanya niwe hapa nilipo hii leo

“Hivyo sina kinyongo na yeyote pale Chelsea, hata meneja Guus Hiddink bado ninaamini ni mtu mwema kwangu, japo alinipa wakati mgumu tangu alipowasili klabuni hapo” Alisema Ramies.

Ramires alipokua Chelsea tangu mwaka 2010 alifanikiwa kucheza michezo 160 na kufanikiwa kufunga mabao 17.

Toni Kroos Anasaka Chaka La Kujifichia Msimu Wa 2016-17
Dudu Baya alipuka tena, adai Bora Chidi Benz Afe