Uongozi wa klabu ya Ihefu FC umekamilisha dili la kumsajili aliyekua kiungo wa klabu za Young Afrcans na Mbeya Cuty Raphael Daudi, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kukiboresha kikosi cha klabu hiyo inayoshiriki kwa mara ya kwanza msimu huu 2020/21.

Ihefu FC wamedhamiria kufanya mabadiliko kwenye kikosi chao katika kipindi cha dirisha dogo la usajili ambacho kitafungwa rasmi hii leo, itakapofika mishale ya saa tano na dakika hamsini na tisa usiku.

Usajili wa kiungo huyo umechagizwa na kocha Zubeir Katwila, ambaye alijitoa muhanga kwa kukubali kuwa mkuu wa benchi la ufundi la Ihefu FC akitokea Mtibwa Sugar mwezi Oktoba mwaka 2020.

Kiungo Daud anajiunga na Ihefu FC kama mchezaji huru, na anatarajiwa kuwa sehemu ya wachezaji ambao wataongeza chachu ya ushindani kwenye kikosi cha klabu hiyo ya mkoani Mbeya.

Daud alijiunga na Young Africans Juni 30, mwaka 2017 na kuichezea mpaka msimu uliopita wa 2019/20 kabla ya kuachwa mwanzoni mwa msimu huu.

Daud pia alikuwemo kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichocheza michuano ya ukanda wa kusini mwa Afrika (COSAFA Castle) na kutwaa Medali ya Shaba baada ya ushindi wa penati 4-2, Julai 7 mwaka 2017 dhidi ya Lesotho kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg.

FC Platinum: Chikwende yupo Dar, Tanzania
Maalim Seif ameokoa ndoa za watu