Beki wa klabu bingwa barani Ulaya Real Madrid Raphael Varane, amesema haikua kazi rahisi kuikataa ofa ya kujiunga na aliyewahi kuwa meneja wake huko Estadio Santiago Bernabeu Jose Mourinho, ambaye kwa sasa anakinoa kikosi cha Man Utd.

Varane alikua miongono mwa wachezaji waliokua wanawaniwa na Mourinho wakati wa dirisha la usajili wa majira ya kiangazi ambao ulihitimishwa usiku wa kuamkia Septemba Mosi.

Akizungumzia na kituo cha televisheni cha nchini Ufaransa Canal+, Varane amesema alitafakari kwa kina juu ya ofa hiyo, ambayo kwake aliamini huenda ingemuweka katika ramani nyingine ya soka kimafanikio, lakini alifanya maamuzi ya kuendelea kubaki na kikosi cha Real Madrid.

“Ni kweli niliikataa ofa ya Man Utd, na ninaamini maamuzi yangu yalikua sahihi japo ulimwengu ulitambua huenda nilifanya makosa ya kugoma kuondoka mjini Madrid katika kipindi hiki, ambacho Mourinho alionyesha kunihitaji,”

“Mara zote nimekua nikionyesha hisia za kuipenda Real Madrid, kwa sababu nimekua kwenye klabu hiyo kwa kipindi kirefu, na mazingira yaliopo yanaendelea kunishawishi kubaki kwa miaka mingine zaidi.”

“Natambua kwa nini Mourinho alihitaji nijiunge Man Utd, lakini sikuona umuhimu huo kwa sasa, japo ilikua vigumu kumkatalia na kuendelea kubaki kwenye kikosi cha Real Madrid, kwangu ninaona ni jambo ambalo ni sahihi.”

Varane alisajiliwa na Jose Mourinho wakati akikiongoza kikosi cha Real Madrid mwaka 2011, akitokea nchini kwao Ufaransa alipokua akiitumikia klabu ya Lens.

Khedira: Schweinsteiger Hastahili Kutendewa Hivi
Picha: Waziri Mkuu awasili Dodoma kwaajili ya Bunge