Beki wa klabu ya Real Madrid pamoja na timu ya taifa ya Ufaransa, Raphael Varane ataukosa mchezo wa hatua ya fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya pamoja na fainali za Euro 2016, kufuatia majeraha ya misuli ya paja yanayomkabili kwa sasa.

Varane alifanyiwa vipimo jana, na amebainika ana tatizo kubwa la maumivu wa misuli ambayo hayawezi kupona katika kipindi hiki kifupi kabla ya fainali za Euro 2016.

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ufaransa Didier Deschamps, tayari ameshamuondoa kwenye kikosi chake na amemuita mlinzi wa klabu ya Sevilla, Adil Rami kama mbadala wake.

Didier Deschamps, amesema amejiridhisha Raphaël Varane hatoweza kuwa sehemu ya kikosi chake ambacho kitakuwa mwenyeji wa fainali za Euro 2016, na amesikitishwa na majeraha yaliyomfika beki huyo mwenye umri wa miaka 23.

Kutokana na hali hiyo, inadhihirisha wazi kwamba msimu wa 2015-16 kwa Rafael Varane umefikia tamati, hivyo hana budi kusubiri msimu wa 2016-17 ambao utashuhudia akirejea tena katika majukumu yake huko mjini Madrid.

Mwishoni mwa juma hili Real Madrid watapambana na Atletico Madrid katika mchezo wa hatua ya fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya mjini Milan nchini Italia.

PICHA 9 KUTOKA ZAMBIA MKUTANO WA ADB, MAJALIWA AMWAKILISHA JPM
Kikosi Cha Misri Kitakachoivaa Taifa Stars Chatajwa